19 Juni 2019 - 09:57
Sadiq Khan: Trump ni nembo ya ubaguzi duniani

Meya wa jiji la London amemtaja rais wa Marekani kuwa nembo ya wabaguzi na mirengo ya kulia yenye misimamo mikali.

(ABNA24.com) Meya wa jiji la London amemtaja rais wa Marekani kuwa nembo ya wabaguzi na mirengo ya kulia yenye misimamo mikali.

Sadiq Khan amejibu matamshi ya kukurupuka ya  Rais Donald Trump wa Marekani ambaye amemtaja  kiongozi huyo wa Uingereza kuwa ni "maafa" na "fedheha kwa taifa la Uingereza." Sadiq Khan amesema kuwa Trump anapasa kutoa maelezo kuhusu jumbe zake za Twitter kwa sababu jumbe hizo zimechangia pakubwa katika kueneza ubaguzi na misimamo mikali duniani. Meya wa London ameongeza kusema kuwa Trump amebadilika na kuwa nembo ya ubaguzi na kuongezeka vitendo vya mabavu kote duniani iwe ni huko Uingereza au katika nchi nyingine duniani.

Khan amesisitiza kuwa Donald Trump anapasa kujibu swali hili kuwa ni kwa nini anaeneza jumbe za Twitter za wanaharakati wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali na zile za wabaguzi? Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Donald Trump aliandika jumbe katika ukurasa wake wa Twitter akimtaja Sadiq Khan kuwa ni 'maafa' na 'fedheha' kwa taifa la Uingereza ambaye analiangamiza jiji la London.



/129