(ABNA24.com) Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei siku ya Jumatatu aliupokea ujumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HaMAS). Katika mazungumzo na ujumbe huo, Ayatullah Khamenei alisisitiza kuwa, kadhia ya Palestina ndiyo kadhia nambari moja na ndilo suala muhimu zaidi kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekusifu kusimama imara na muqawama wa kustaajabisha wa wananchi wa Palestina pamoja na makundi ya muqawama likiwemo la Hamas na akasisitiza kwa kusema: Ushindi haupatikani bila muqawama na mapambano, na kwa mujibu wa ahadi isiyokhalifu ya Allah, sisi tunaitakidi kuwa, hatima ya maudhui ya Palestina bila shaka itakuwa kwa manufaa ya watu wa Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu.
Taifa la Palestina hadi sasa limesimama imara kuzikabili njama mbali mbali; na kusimama imara huko kumetokana na kuwa na moyo wa matumaini ya kupata ushindi na imani juu ya hakika kwamba, kuendeleza mapambano na muqawama, na kuwa na matumaini juu ya mustakabali, ndiyo njia pekee ya kuikomboa Palestina kutoka kwenye makucha ya uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa adui Mzayuni.
Japokuwa vuguvugu la muqawama hadi sasa limeweza kuzima mipango na njama nyingi za Wazayuni za kuigawa Palestina, lakini ukweli ni kwamba suala la Palestina ni jihadi kubwa ya taifa linalopigania kupata haki yake ya kihistoria.
Ni kwa sababu hiyo, kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, suala la Palestina lingali limebaki kuwa kadhia kuu ya masuala ya kisiasa ya umma wa Kiislamu; na Waislamu wote wana wajibu wa kufanya bidii na juhudi kubwa kwa ajili ya kulikomboa na kuliokoa taifa la Palestina.
Kuhusiana na suala hilo, katika mazungumzo yake na ujumbe wa Hamas, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mzaha na nchi yoyote katika kadhia ya Palestina; na akakumbusha kwa kusema: Moja ya sababu muhimu za uadui inaofanyiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni maudhui ya Palestina; lakini uadui huo na mashinikizo yanayotolewa, hayataifanya Iran irudi nyuma katika misimamo yake kuhusiana na kadhia ya Palestina, kwa sababu kuiunga mkono Palestina ni suala la kiitikadi na kidini.
Inasikitisha kuona kwamba, kutokana na baadhi ya harakati za usaliti, ulegevu na udhaifu wa baadhi ya tawala za nchi za Kiislamu, leo hii taifa la Palestina limejikuta likikabiliwa na njama nyingine mpya ya Uzayuni na Marekani iliyopewa jina la "Muamala wa Karne."
Majid Safaa Taj, mtaalamu wa masuala ya Palestina ameyachambua malengo ya Marekani kupitia mpango wa "Muamala wa Karne" kwa kusema:
"Israel imedhamiria kuifuta haki ya Wapalestina kurejea kwenye ardhi yao kwa kutumia mpango wa Muamala wa Karne; na mbali na Marekani, Saudi Arabia pia inafuatilia utekelezaji wa mpango huo."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amebainisha malengo ya njama hiyo chafu na ovu kwa kusema:
Lengo la njama hii hatari ni kufuta utambulisho wa Palestina miongoni mwa wananchi na vijana wa Kipalestina; kwa hivyo inapasa kukabiliana na nukta hii hii ya msingi, kwa kutowaruhusu waufute utambulisho wa Palestina kwa kutumia pesa.
Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, moja ya mambo ya lazima kwa ajili ya mafanikio ya mapambano hayo ni kuendeleza misimamo imara, kusimama kidete na kuhisi kuwa kuna upigaji hatua; nukta ambayo Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameiashiria katika barua yake kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amekumbusha kuhusu nukta hiyo kwa kusema: "Si miaka mingi nyuma Wapalestina walikuwa wakipambana kwa mawe, lakini leo hii badala ya mawe, wamejizatiti kwa makombora yanayolenga shabaha iliyokusudiwa, na hii ndiyo maana ya kuhisi kumepigwa hatua."
Nasaha na miongozo aliyotoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika mazungumzo na ujumbe wa Hamas hapo jana imetoa mwanga wa wazi na kuonyesha muelekeo sahihi wa njia ya kufuatwa na harakati ya muqawama hadi kufikia ushindi kamili, na kudhihirisha ukweli kwamba, historia inaweza kujirudia; kwa sababu kwa mujibu wa utaratibu na kaida aliyoweka Allah, ushindi wa wananchi wa Palestina na kurejea ardhi hiyo tukufu mikononi mwa UIimwengu wa Kiislamu si jambo la ajabu na lisiloweza kuthibiti.
Katika kubainisha uhakika huo, Ayatullah Khamenei alisema: Miaka 40 nyuma, hakuna mtu ambaye angeweza kuamini kama nchini Iran, iliyokuwa kitovu cha satua na tumaini la Marekani, ungeshika madaraka utawala wa kidini, na ubalozi wa Israel Tehran ungegeuzwa kuwa ubalozi wa Palestina; lakini jambo hilo ambalo mtu asingeweza kuamini lilithibiti. Kwa hivyo kuthibiti mambo ambayo kidhahiri yanaonekana kuwa ni ya ajabu ni jambo linalowezekana.
Hakuna shaka kuwa hali ya kadhia ya Palestina leo hii haiwezi kulinganishwa na huko nyuma. Muqawama una nguvu na uwezo mkubwa wa kukabiliana na maghasibu wa Kizayuni na umesimama imara kupambana na utawala haramu wa Israel na wala hautaruhusu katu utawala huo wa Kizayuni ufikie malengo yake maovu. Ni kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Ikiwa sisi sote tutatekeleza majukumu yetu, ni hakika kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu itathibiti tu.../
/129