25 Septemba 2019 - 08:15
Rais Rouhani: Kama Trump anataka mazungumzo na Iran arekebishe kwanza yote aliyoyaharibu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kama kweli rais wa Marekani, Donald Trump anataka mazungumzo na Iran, anapaswa kabla ya jambo lolote arejeshe kwanza imani ya taifa hili aliyoipoteza.

(ABNA24.com) Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kama kweli rais wa Marekani, Donald Trump anataka mazungumzo na Iran, anapaswa kabla ya jambo lolote arejeshe kwanza imani ya taifa hili aliyoipoteza.

Rais Rouhani amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya Fox News ya nchini Marekani pambizoni mwa kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kujibu swali la mwendesha vipindi wa televisheni hiyo, Chris Wallace, kuhusu uwezekano wa yeye kuonana na Donald Trump hata kwa bahati mbaya kwamba, lililo muhimu kabla ya jambo lolote, ni Trump kurejesha imani ya taifa la Iran aliyoipoteza kwa hatua zake za kiuadui dhidi ya taifa hilo.

Ameongeza kuwa, Marekani ni muungaji mkono wa ugaidi katika eneo la Asia Magharibi na kwamba popote ambapo nchi hiyo inaweka mguu wake magenge ya kigaidi hupata nguvu kwenye eneo hilo.

Katika upande mwingine, Rais Rouhani alisema jana katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson huko New York, Marekani kwamba nchi za Ulaya zinapaswa kuheshimu ahadi zao ndani ya mapatano ya nyuklia, JCPOA, na si kutoa maazimio yaliyotegemea tuhuma zisizo na mashiko dhidi ya Iran.

Vile vile ameilaumu Uingereza kwa kuzembea kutekeleza ahadi zake za kuirahisishia Iran njia za kufaidika na mapatano ya JCPOA na kusisitiza kuwa, inachotaka Tehran ni nchi za Ulaya kuheshimu tu ahadi zao, ikiwemo kufungua kanali ya mabadilishano ya fedha maarufu kwa jina la INSTEX.



/129