Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kikao cha Vienna mara hii kinatarajiwa kufanyika katika hali ambayo, Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) wiki iliyopita zilifanya mazungumzo yaliyokuwa na natija nzuri hapa mjini Tehran ambapo Iran ilifikia makubaliano mapya na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusiana na suala zima la kupanua ushirikiano.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Iran itatoa fursa kwa hiari kukaguliwa maeneo mawili yaliyoainishwa na wakala wa IAEA na pia itarahisisha shughuli za ukaguzi wa wakala huo ili kuyapatia ufumbuzi masuala hayo. Pande mbili za Iran na IAEA zimekubalina pia kuhusu tarehe ambayo wakala huo utapaswa kufika katika maeneo hayo yaliyoainishwa na kufanya ukaguzi wake. Katika uwanja huo, Helga Schmid, Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ametathmini makubaliano hayo kama habari njema na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Katika kikao chetu kijacho cha Kamisheni ya Pamoja, tutaendeleza juhudi zetu za kuyalinda na kuyabakisha makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Sayyid Abbas, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa tayari amewasili Vienna mji mkuu wa Austria ambapo kabla ya kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA alitarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia (IAEA), baadhi ya viongozi wa viongozi wa jumbe zitakazoshiriki katika kikao cha kesho pamoja na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Austria. Mazungumzo hayo yanaendelea katika hali ambayo, ushahidi na ishara nyingi zinaonyesha kuwa, siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa za Marekani dhidi ya Iran zimekabiliwa na mkwamo.
Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuhusiana na jambo hilo kupitia ujumbe wake aliouandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: “Ninasema wazi na bayana kwamba, sisi tunapaswa kuyalinda na kuyabakisha makubaliano haya ya nyuklia ya JCPOA kwa sababu mbili: Mosi ni kuwa, hakuna chaguo mbadala la makubaliano haya. Na pili ni kuwa, hii fikra kwamba, eti tunaweza kuwa na makubalino mengine na tuyaite ‘makubaliano ya Trump’ katu ni jambo lisilowezekana. Imepita miaka 12 ambapo hitilafu zimewekwa kando na kupelekea kufikiwa makubaliano haya…”
Licha ya upinzani na ukosoaji wa kila upande, Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa mara nyingine tena amejaribu kutumia jukwaa la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la siasa za Washington na kwa utendaji huo ametoa ombi la kutekelezwa utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", kwa kimombo "Trigger Mechanism" kupitia barua aliyoituma kwa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo. Hata hivyo, juhudi hizo za mfa maji ambaye haishi kutapatapa nazo zimegonga mwamba ambapo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilitangazwa kuwa, kwa kuzingatia upinzani wa akthari ya wanachama dhidi ya takwa hilo la Marekani, haiwezekani kuchukuliwa hatua nyingine.
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran kabla ya hapo alikuwa ameuandikia barua Mwenyeikiti wa Kiduru wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kueleza bayana kwamba, kutokana na sababu na hoja mbalimbali, Marekani haina haki ya kuhuisha vikwazo dhidi ya Iran ambavyo vilifutwa huko nyuma.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani ilihitimisha ushiriki wake kama mwanachama wa makubaliano ya JCPOA na kimsingi haina haki yoyote ile ya kisheria ya kutumia utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", Aidha Mei 11 mwaka 2018, iliwapa taarifa washirika wote wa JCPOA kwamba, nchi hiyo hatashiriki tena katika vikao vinavyohusiana na makubaliano hayo.
Hivi sasa pia kushadidi upinzani wa siasa za Marekani zilizo dhidi ya makubaliano ya JCPOA ni ujumbe wa wazi kabisa kwamba, stratijia ya upande mmoja ya Washington haikubaliwi tena na jamii ya kimataifa. Kama alivyosema Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kabla ya kikao cha Iamisheni ya pamoja ya JCPOA mjini Vienna kuwa: Inatarajiwa sauti moja iliyokuwako katika JCPOA itapazwa na kusikika dhidi ya ukiukaji mambo na uchukuaji maamuzi wa upande wa utawala wa Marekani.
342/