Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Uvamizi huo umetekelezwa usiku wa kuamkia leo Alhamisi baada ya wakuu wa utawala wa Israel kudai kuwa kombora kutoka Syria lilitua karibu na kituo cha nyuklia cha siri cha utawala huo cha Dimona.
Shirika Rasmi la Habari la Syria (SANA) limenukulu duru za kijeshi zikisema kuwa, hujuma hiyo mpya ya Israel imewajeruhi wanajeshi wanne na kuharibu baadhi ya maeneo.
Taarifa hiyo imesema: "Takribani saa saba na dakika 38 usiku, adui Muisraeli ametekeleza hujuma ya anga kwa makombora ambayo yalitokea upande wa milima ya Golan ya Syria, inayokaliwa kwa mabavu, na kulenga eneo la mji wa Damascus."
Taarifa hiyo imesema makombora hayo yametunguliwa na mfumo wa kujihami angani wa Syria. Mapema jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilitangaza kuwa kombora la Syria lililipuka kusini mwa Israel na kupelekea hali ya tahadhari ya kivita kutangazwa katika eneo hilo ambalo liko karibu na kituo chenye usiri mkubwa cha nyuklia cha Dimona.
Katika kujibu hujuma hiyo iliyodaiwa kutekelezwa na Syria, Israel imesema imelenga mifumo ya makombora ya Syria ikiwa ni pamoja na mfumo uliotumika kuvurumisha kombora lililotua karibu na Dimona. Serikali ya Syria haijatoa taarifa rasmi kuhusiana na madai hayo ya Israel.
Jeshi la Israel limedai kombora hilo ni aina ya SA-5 na kusema kuwa limevurumishwa na Jeshi la Syria na kwamba liliruka umbali wa kilomita 200 kutoka mpaka wa Syria hadi eneo la Dimona. Jeshi hilo limekiri makombora ya ulinzi wa anga ya Israel hayakuweza kutungua kombora hilo.
342/