Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Antonio Guterres amesema hayo wakati alipokutana na Rais Xi Jinping wa China na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo Wang Yi pambizoni mwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mjini Beijing.
Duru za karibu na mazungumzo hayo zinasema kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea matumaini yake kwamba mawasiliano kati ya ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu na maafisa wa serikali ya China, yataruhusu kufanyika ziara 'yenye kuaminika' ya kamishna huyo nchini China, ikiwa ni pamoja na jimbo la Xinjiang.''
Asasi mbalimbali zimekuwa zikilaani ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali ya China dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uighur katika jimbo la Xinjiang kaskazini mwa China na kusema kuwa, ukandamizaji huo mkubwa haujawahi kushuhudiwa nchini humo.
Hata hivyo serikali ya China imekuwa ikikana tuhuma dhidi yake za mateso dhidi ya Waislamu, ikisema kuwa inawapatia mafunzo katika kambi ili waondokane na fikra za itikadi kali. Wauighur wanaishi kaskazini magharibi mwa China katika jimbo lenye mamlaka yake ya ndani la Xinjiang.
Taarifa zaidi zinasema, Maimamu na viongozi wa Kiislamu wasiopungua 630 wamekamatwa nchini China tangu mwanzoni mwa operesheni ya kuwakamata iliyoanza katika jimbo la Xinjiang mwaka 2014 na kwamba, Maimamu 18 walikufa muda mfupi tu baada ya kukamatwa hali ambayo inatia wasiwasi kwamba, huenda waliuawa.
342/