8 Oktoba 2022 - 20:59
Mkakati erevu wa serikali ya Sana'a baada ya kumalizika usitishaji vita; kulenga sekta ya nishati

Kufuatia kushindwa mapatano ya kurefusha usitishaji vita nchini Yemen, msemaji wa jeshi la nchi hiyo ameonya kuwa usalama wa uwekezaji katika nchi mbili za Saudi Arabia na Imarati uko hatarini.

Mwaka wa nane wa vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen unakaribia kumalizika. Yemen inakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu kutokana na vita hivyo. Baada ya Umoja wa Mataifa kukosolewa vikali kwa kushindwa kusimamisha vita na wakati huo huo Saudi Arabia kushuhudia mashambulizi makali ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Wayemen, hatimaye usitishaji vita ulifikiwa kati ya pande hizo ambapo ulianza kutekelezwa kuanzia Aprili mwaka huu wa 2022.

Makubaliano hayo yalidumu kwa muda wa miezi miwili na kurefushwa mara mbili mwezi Juni na Agosti, lakini yalimalizika tarehe 2 Oktoba ambapo pande zinazozozana zilishindwa kurefusha tena mapatano hayo kutokana na uvurugaji wa muungano wa Waarabu na pia ukiukwaji wa mara kwa mara wa makubaliano hayo na Saudia. Mkakati wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen katika kukabiliana na ukiukaji huo umekuwa ni kuchukua hatua zinazafaa kwa ajili ya kukabiliana nao.

Kwa hakika sababu kuu ya kushindwa usitishaji vita huo ni hatua ya Saudia na Imarati ya kuizuia Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kunufaika na mapato ya mafuta, jambo ambalo limeifanya serikali ya Sana'a ikabiliwe na matatizo mengi katika kuwalipa mishahara wafanyakazi wake. Kwa kuzingatia hayo, Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa vikosi vya jeshi la Yemen ametoa maonyo mawili kwa wavamizi na wawekezaji wa Saudi Arabia na Imarati.

Amezionya nchi hizo wavamizi kwa kusema: "Mara tu baada ya kumalizika kipindi cha usitishaji vita nchini Yemen na iwapo taifa halitafikia matakwa yake ya haki, tutakushughulikieni vilivyo. Vikosi vyetu vya kijeshi vinajiandaa kwa ajili ya hatima yoyote ile katika saa zijazo."

Siku ya Jumanne usiku, Yahya Saree aliyataka mashirika ya kigeni yanayowekeza huko Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kuhamisha uwekezaji huo na kuupeleka sehemu nyingine. Alisisitiza kwa kusema: "Kuwekeza Imarati na Saudi Arabia itakuwa hatari kubwa." Yahya Saree pia alisema Jumapili jioni: "Kwa sababu nchi vamizi hazizingatii usitishaji vita na haziruhusu taifa la Yemeni kunufaika na rasilimali za mafuta ili kulipa mishahara ya wafanyikazi wake, tunayapa mashirika ya mafuta yanayofanya kazi nchini Saudi Arabia na Imarati fursa ya kubadilisha mipango yao na kuondoka katika nchi mbili hizo." Ameendelea kusema: "Iwapo Saudi Arabia na Imarati zitasisitiza kuwanyima watu wa Yemen rasilimali na mapato yao, majeshi yetu ya kijeshi yana uwezo wa kuzinyima pia tawala hizo mapato yao."

Mkakati wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen wa kukabiliana na zama za baada ya kumalizika usitishaji vita ni mkakati erevu na wa busara. Mapato ya serikali za Saudi Arabia na Imarati yanategemea rasilimali za mafuta moja kwa moja. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, jeshi la Yemen mara kadhaa limelenga vituo vya mafuta vya Imarati na hususan Saudi Arabia kwa kushambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani taasisi za mafuta za nchi hizo na kuzisababishia hasara kubwa.

Kwa upande mwingine, Riyadh na Abu Dhabi zimelipa zingatio maalumu suala la uwekezaji wa kigeni, na nchi zote mbili zinaona kuwa zinaweza kufikia ndoto yao ya kiuchumi iwapo tu zitafanikiwa kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni katika sekta ya nishati na mafuta. Bila shaka kulengwa usalama wa Saudi Arabia na Imarati kunaweza kuathiri pakubwa uwekezaji mpya na uwepo wa mashirika ya kigeni katika nchi hizo. Wakati huo huo, kulengwa vituo vya nishati vya nchi hizo pia kutaathiri usambazaji na bei ya nishati katika masoko ya kimataifa. Iwapo hilo litatimia, ni wazi kuwa jamii ya kimataifa italazimika kufanya juhudi zaidi kwa lengo la kufikia usitishaji mapigano wenye kutegemewa na imara zaidi nchini Yemen.