Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA-, Waumini wa Madhehebu ya Shia Ithna Ashari, Jijini Dar-es-Salam, Tanzania, wamejitokeza kwa wingi katika Mkesha wa Usiku wa 19 wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, uliohuishwa katika Hawza ya Imam Sadiq (a.s), ndani ya Masjidul Ghadir, iliyopo Kigogo, Post, Dar-es-Salam, Tanzania.
Mkesha huu umeambatana na Majlis ya kumbukumbu ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (a.s) kupigwa Upanga wenye sumu kali kupitia muovu Ibn Muljim. Majlis hiyo ilisomwa na Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, ambaye amebainisha kuwa Usiku huu wa 19 wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ndio Usiku ambao Amirul Muuminina Ali (a.s) alipigwa upanga kichwani akiwa ndani ya Msikiti na akiswali Swala ya Al-fajiri.
Amebainisha kuwa: Adui Ibn Muljim (laana iwe juu yake), aliyempiga Imam Ali (a.s) kwa upanga wenye sumu kali, alijua kuwa hawezi kupambana na Imam Ali (a.s) akiwa nje ya Msikiti, hivyo akaona mbinu aliyokuwa nayo ni kumuwinda akiwa katika ibada (swala). Anasema: Nilimuwinda Ali -a.s- kwa muda mrefu na nilijua kuwa ili kumuua Ali -(a.s)- ni lazima kumuwinda akiwa katika Swala, kwani awapo katika swala huwa mwili wake na hisia zake zinatoweka Duniani, na anazungumza na Mola wake Mtukufu kama vile hayupo Duniani".
Na hapo ndipo Ibn Muljim (lana iwe juu yake) alipopata fursa ya kumpiga upanga wenye sumu kali kichwani, kwa upanga huo ikawa ndio sababu ya Shahda ya Amirul-Muuminin (amani iwe juu yake).
Waumini wakiwa katika Mkesha wa 19 wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wakijishughulisha na ibada na dua mbalimbali, ndani ya Masjid Ghadir, Kigogo Post, Dar-es-Salam, Tanzania, sambamba na kuhuisha kumbukumbu ya kupigwa Upangwa kwa Kiongozi wa Waumini, Ali bin Abi Talib (a.s), ambao ndio ilikuwa sababu ya Kifo chake cha Kishahidi.
Majlish hii imeambatana na kauli mbiu isemayo: "Amani ya Palestina ni Amani ya Tanzania".
Your Comment