26 Julai 2025 - 21:14
Ayatollah Sistani Aitaka Dunia ya Kiislamu Kuchukua Hatua Haraka Kuhusu Njaa Inayoikumba Gaza

Kauli ya Ayatollah Sistani inakuja wakati ambapo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaonya kuwa njaa inasambaa kwa kasi kote Gaza, huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikionesha kuwa karibu watu nusu milioni wanakumbwa na viwango vya juu vya njaa kali.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kiongozi mashuhuri wa Kishia kutoka Iraq, Ayatollah Al-Udhma Sayyid Ali al-Sistani, ameeleza masikitiko makubwa juu ya hali mbaya ya kibinadamu inayozidi kuzorota katika Ukanda wa Gaza, hasa kutokana na njaa kali inayosambaa, na kutoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kuchukua hatua madhubuti kuzuia janga hilo la kutisha.

Katika taarifa yake aliyotoa Ijumaa jioni, Ayatollah Sistani alisema:

"Baada ya karibu miaka miwili ya mauaji na uharibifu usiokoma, yaliyosababisha vifo na majeruhi kwa mamia ya maelfu ya watu pamoja na kubomolewa kwa miji na majengo ya makaazi, watu wa Palestina waliodhulumiwa katika Ukanda wa Gaza sasa wanaishi katika mazingira ya kutisha."

Ameonya kuwa njaa imeenea kwa kiwango kikubwa mno na hakuna sehemu yoyote ya jamii iliyobaki salama dhidi ya athari zake.
Ayatollah Sistani alisisitiza kuwa haiwezi kutarajiwa chochote kutoka kwa utawala wa Israel isipokuwa unyama wa kusikitisha unaolenga kuwaangamiza Wapalestina.

Alieleza kuwa jamii ya kimataifa, hususan mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, yana wajibu wa kimaadili na kibinadamu kuhakikisha janga hili haliendelei. Ameyataka mataifa hayo kuharakisha juhudi za kimataifa kumaliza maangamizi haya na kulazimisha utawala wa Tel Aviv pamoja na washirika wake kuruhusu kuingizwa kwa chakula na mahitaji mengine ya msingi kwa raia wa Gaza haraka iwezekanavyo.

Kauli ya Ayatollah Sistani inakuja wakati ambapo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaonya kuwa njaa inasambaa kwa kasi kote Gaza, huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikionesha kuwa karibu watu nusu milioni wanakumbwa na viwango vya juu vya njaa kali.

Zaidi ya Wapalestina 100 — wengi wao wakiwa watoto — wameripotiwa kufariki kutokana na njaa katika wiki chache zilizopita, huku hospitali zikikabiliwa na changamoto kubwa kuwahudumia watoto walioathirika kwa utapiamlo mkali.

Misaada ya kibinadamu bado inazuiwa vikali, huku vikosi vya Israel vikihujumu au kuzuia misafara ya misaada inayojaribu kufika kaskazini na kati ya Gaza.
Mashirika ya kimataifa kama Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) yametaja hali hii kuwa ni njaa iliyosababishwa kwa makusudi na mwanadamu, na yametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiwekea shinikizo Israel kuondoa mzingiro huo mara moja.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha