27 Agosti 2025 - 23:29
Troika ya Ulaya Katika Hatua za Mwisho za Kurejesha Vikwazo vya Umoja wa Mataifa Dhidi ya Iran

Troika ya Ulaya iko karibu kuanzisha upya utaratibu wa “snapback” dhidi ya Iran, hatua ambayo inaweza kukaribia kumaliza makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- wanadiplomasia wanne wametangaza kwamba huenda nchi za Troika ya Ulaya (Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) kesho Alhamisi zikaanza mchakato wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Hata hivyo, nchi hizo zinatarajia kuwa Iran ndani ya siku 30 itatoa ahadi kuhusu mpango wake wa nyuklia zitakazozishawishi kuahirisha hatua za moja kwa moja.

Katika muktadha huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani leo Jumatano ametangaza kwamba Ufaransa, Uingereza na Ujerumani bado ziko tayari kuanzisha utaratibu wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Msimamo huu umefuata kikao cha pande tatu na Iran huko Geneva siku ya Jumanne, kikao kilichofanyika kwa lengo la kufufua juhudi za kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Msemaji wa Kijerumani katika mkutano na waandishi wa habari ameongeza kuwa, licha ya kutofikiwa matokeo ya mwisho katika mazungumzo hayo, chaguo la kurejesha vikwazo bado lipo mezani, lakini nchi tatu za Ulaya zitaendelea kutafuta suluhisho la kidiplomasia.

Ahadi ya Iran kwa diplomasia

“Kazem Gharibabadi,” Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jana Jumanne alisisitiza kujitolea kwa nchi yake kwa diplomasia na suluhisho lenye manufaa kwa pande zote, na kusema kwamba sasa umefika wakati wa Troika ya Ulaya na Baraza la Usalama kuchukua uamuzi sahihi.

Ameongeza kuwa pande hizo zimejadili mitazamo yao kuhusu Azimio namba 2231 la Baraza la Usalama; azimio linalounga mkono makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.

Kikao cha Geneva kilijikita katika kujadili madai ya Magharibi kuhusu kurejea kwa ukaguzi wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Kimataifa (IAEA) kwenye mitambo ya nyuklia ya Iran, na lengo lake lilikuwa kufufua njia ya kidiplomasia ili kufikia makubaliano au kukabiliana na kurejeshwa kwa vikwazo vilivyokuwa vimeondolewa kwa mujibu wa makubaliano ya 2015.

Muda wa mwisho na kurejea kwa wakaguzi

Mapema mwaka huu, nchi za Ulaya zilikubaliana na Marekani kwamba endapo Iran hadi mwisho wa mwezi Agosti haitakuwa imejibu masharti maalum, basi utaratibu wa snapback utafanyiwa kazi. Masharti hayo ni pamoja na kurejea kwa mazungumzo na Marekani, kuruhusu wakaguzi wa IAEA kufikia mitambo ya nyuklia ya Iran, na kubainisha hatima ya zaidi ya kilo 400 za urani yenye kiwango cha juu cha uenezaji.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Kimataifa, leo Jumatano ametangaza kwamba wakaguzi wa shirika hilo baada ya kutokuwepo zaidi ya wiki 7 wamekuwa wakirejea Iran na wanakusudia kuanza upya shughuli zao.

Kwa upande wake, Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza kwamba kuingia kwa wakaguzi wa shirika hilo nchini kumeamuliwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na lengo lake ni kusimamia mchakato wa kubadilisha mafuta katika kituo cha nyuklia cha Bushehr.

Amesisitiza kwamba kinyume na madai ya baadhi ya wawakilishi, sheria iliyopitishwa na Bunge haijavunjwa. Kwa mujibu wa sheria hiyo, ushirikiano na shirika hilo unategemea uamuzi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na maombi yote ya shirika hilo lazima yawasilishwe kwa baraza hilo.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Iran leo Jumatano wamepinga kuruhusu ukaguzi katika kituo cha nyuklia cha Bushehr na Kituo cha Utafiti cha Tehran na wameona kuwa ni kinyume na sheria iliyopitishwa na Bunge. Sheria hiyo ambayo ilipitishwa Juni 26 na kuidhinishwa pia na Baraza la Kulinda Katiba, inalazimisha serikali kuzuia kuingia kwa wakaguzi wa shirika hilo na kusitisha shughuli zote za ukaguzi. Iran imekituhumu Shirika la Nishati ya Atomiki la Kimataifa kwa kushiriki katika shughuli za ujasusi na kutoa mazingira ya mashambulio ya Israel na Marekani.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha