Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sheikh Mahdi al-Sumayda‘i, Mkuu wa Darul Ifta ya Iraq, katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, alisema:
Mtume wa Uislamu (saw) amesema: "Damu ya kila Muislamu ni haramu kwa Muislamu mwenzake." Hata hivyo, tunashuhudia mauaji yasiyo na idadi yanayofanywa na adui wa Kizayuni huko Gaza na sehemu nyingine za dunia, lakini kwa masikitiko makubwa, hakuna sauti inayosikika kutoka kwa nchi nyingine.
Mufti wa Jamhuri ya Iraq alisisitiza kuwa Umma wa Kiislamu kwa sasa uko katika hali ngumu, na akabainisha:
"Waislamu wote wanapaswa kusimama kwa sauti moja na kwa mshikamano dhidi ya adui. Adui, kwa sababu ya majivuno na kiburi chake kisicho na msingi, amejipa ujasiri wa kuwatisha viongozi wa nchi za Kiislamu – hali hii imetokea kwa sababu mataifa ya Kiislamu yamezama katika usingizi mzito wa ghafla."
Sheikh al-Sumayda‘i alieleza kuwa:
"Waislamu hivi sasa wametengana na wanauana wao kwa wao, jambo ambalo limewapa kisingizio Wamagharibi kudai kuwa Waislamu wanajiharibu wenyewe."
Akiendelea, alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awaamshe Waislamu kutoka usingizi wa ghafla, ili waweze kubeba jukumu zito lililo juu yao. Pia alimuomba Mwenyezi Mungu kuufanikisha mkutano huu katika malengo yake, na kwamba umoja urejee tena miongoni mwa Waislamu, ili wawe wamoja na wenye mshikamano.
Mwisho wa hotuba yake, Mufti wa Ahlus-Sunnah wa Jamhuri ya Iraq alisisitiza:
"Lazima tuseme 'NDIYO' kwa umoja wa Waislamu, na kwa kukataa ubeberu wa kimataifa, tuseme 'HAPANA' kwa Magharibi na mabeberu."
Your Comment