Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- hivi karibuni nchini India, uandishi wa mabango yenye maandishi “Nampenda Muhammad” pamoja na kampeni zinazofanana, ikiwemo za video na mitandaoni, umekumbwa na upinzani kutoka kwa makundi ya Kihindu na ukatili wa polisi.
Asaduddin Owaisi, kiongozi wa chama cha Majlis Ittehad-ul-Muslimeen, alitoa kauli kali akijibu mzozo huo akisema: “Kwa nini tamko la mapenzi na heshima kama hili lichukuliwe kama uchochezi?”
Amesisitiza kuwa kampeni hii ni tendo la upendo na heshima tu, na akauliza: “Kama kundi fulani linasema ‘Nampenda Mahadev (mtakatifu wa Kihindu)’, tatizo liko wapi? Hilo linaweza vipi kuwa kinyume cha taifa? Ni kwa namna gani linaweza kuchochea vurugu?”
Owaisi akiwaeleza waandishi wa habari aliendelea kusema: “Iwapo ni juu ya ‘mapenzi’, kwa nini iwe shida? Kama kuna bango ‘Heri ya Kuzaliwa Waziri Mkuu Modi’, kwa nini isiwepo bango ‘Nampenda Mtume Muhammad (s.a.w)’?”
Aidha, akirejea Kifungu cha 25 cha Katiba ya India, alibainisha kuwa uhuru wa dini ni haki ya kimsingi. Akasema: “Ni kipengele gani cha jambo hili kilicho kinyume cha taifa? Ni sehemu ipi inayochochea vurugu? … Imani ya Mwislamu haikamiliki isipokuwa Mtume Muhammad (s.a.w) apendwe zaidi ya chochote duniani. Tukipinga hili, tunapeleka ujumbe gani kwa dunia?”
Vilevile, alimshutumu vikali gavana na polisi wa jimbo la Uttar Pradesh kwa kuweka vizuizi vya kibaguzi, akisema: “Kamanda wa polisi anasema mabango mapya hayataruhusiwa. Lakini mabango ya ‘Heri ya Kuzaliwa Waziri Mkuu’ au ‘Heri ya Kuzaliwa Waziri wa Jimbo’ yanaruhusiwa. Basi tupitishe sheria kwamba hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuzungumzia mapenzi katika nchi hii.”
Ikumbukwe kuwa siku ya Ijumaa kulifanyika maandamano makubwa ya Waislamu nchini India wakipinga kufunguliwa kesi kwa washiriki wa kampeni hii. Polisi walikabiliana kwa nguvu na vurugu, na kusababisha idadi ya Waislamu kukamatwa.
Your Comment