Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Kimataifa AhlulBayt (a.s) -ABNA- Dkt. Abbas Khamehyar, mshauri wa masuala ya kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dini na Madhehebu, katika kikao maalumu chenye mada: “Athari za kudumu kwa utawala wa chama cha AKP juu ya Uislamu wa kisiasa na mwelekeo wa sera za dini nchini Uturuki”, alieleza kwa kina mabadiliko makubwa ya kisiasa na ya kimfumo yaliyotokea nchini humo katika kipindi cha miaka ishirini tangu chama cha AKP kilipoingia madarakani.
Kikao hiki ambacho kilifanyika leo asubuhi tarehe 28 Aban 1404 kwa juhudi za shirika la habari la ABNA kwa kushirikiana na kituo cha fikra cha Zaviyeh, kilichambua mabadiliko ya utambulisho wa kitaifa, mageuzi katika taasisi za kiserikali na mabadiliko ya sera za mambo ya nje katika kipindi baada ya ukali wa kisekula wa enzi za Kamalisti.
Dkt. Khamehyar alisisitiza kuwa mabadiliko muhimu kabisa ni kudumu kwa chama cha AKP katika mfumo wa kisekula wa Uturuki na kuhamisha Uislamu wa kisiasa kutoka msikitini kuingia ndani ya wizara mbalimbali za serikali. Alifafanua pia mwelekeo mpya wa Uturuki katika masuala ya ndani na nje ya nchi.
Sehemu ya Kwanza: Mageuzi ya Utambulisho wa Jamii na Uislamishaji wa Miundo
1. Uislamishaji wa polepole na wa kimkakati
Dkt. Khamehyar aliuelezea Uislamu wa kisiasa nchini Uturuki kama “mabadiliko ya polepole, yenye busara na yasiyo na mgongano wa moja kwa moja”. Tofauti na nchi nyingi ambazo Uislamu wa kisiasa unasababisha makabiliano na taasisi za kisekula, nchini Uturuki mchakato huu umefanyika hatua kwa hatua na kwa njia zisizo za moja kwa moja:
- Athari katika elimu: Kuongezeka kwa shule za “Imam Hatip” ambazo awali zilikuwa za kuandaa makhatib, lakini sasa zimekuwa njia ya kukuza wasomi wenye mwelekeo wa kidini wanaoingia katika serikali, elimu na jeshi.
- Kuimarika kwa elimu ya Qur’ani: Kuongeza mafundisho ya Qur’ani na elimu ya dini katika shule za umma na vyuo vikuu, jambo ambalo limepunguza kwa taratibu athari za kisekula za enzi za zamani.
- Kuimarika kwa vyombo vya habari vya dini: Kufunguliwa kwa vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali na kuruhusu maudhui ya dini kuingia katika maisha ya jamii.
2. Kuongezeka kwa mtindo wa maisha wa kidini mijini
Mabadiliko haya yamesababisha kuibuka kwa mtindo wa maisha wa kidini hasa mijini:
- Dalili za wazi: Kuongezeka kwa hijabu katika ofisi za serikali na vyuo, migahawa ya halal na usanifu wa Kiislamu katika miradi ya ujenzi.
- Uchumi wa halal: Soko jipya la uchumi wa Kiislamu, likiwemo utalii wa Kiislamu.
Dkt. Khamehyar alitaja hili kuwa “ustadi wa watawala wa Uturuki wa sasa” kwani dini imeweza kuingia katika maisha ya watu bila kuvunja misingi ya kisekula iliyopo kwenye katiba.
3. Utambulisho mpya wa Uturuki: Mchanganyiko wa Uislamu wa kisiasa na utaifa
Mabadiliko haya yameunda utambulisho mpya wenye nguzo tatu:
- Uislamu wa kisiasa: Kurejesha maadili ya dini na kuyafanya sehemu ya utambulisho wa taifa.
- Utaifa mkali: Kurejea kumbukumbu za dola ya Ottoman.
- Nguvu ya kijiopolitiki: Kujiweka kama dola yenye ushawishi katika eneo, kwa misingi ya maslahi yake ya kimkakati.
Sehemu ya Pili: Sera ya Mambo ya Nje kwa Msingi wa Nguvu Laini ya Ottoman
Mageuzi ya ndani yameathiri kwa moja kwa moja sera ya nje ya Uturuki:
1. Kurejesha mamlaka laini ya Ottoman
- Lengo ni kupata nafasi ya uongozi katika ulimwengu wa Kiislamu.
- Ushindani wa kikanda: Kati ya Uturuki na Saudi Arabia & UAE katika uongozi wa Uislamu wa wastani.
- Diplomasia ya majadiliano: Sera ya “migogoro sifuri” (japo ilishindwa), na juhudi za kuwa mpatanishi katika migogoro ya kikanda.
2. Uturuki kama kimbilio la Uislamu wa kisiasa wa Kiarabu
- Baada ya misukosuko ya “Arab Spring”, Uturuki imekuwa makao makuu ya Ikhwanul Muslimin.
- Imelitumia wazo la Ikhwan kuathiri tawala za Kiarabu, hususan Saudi, UAE na Misri.
- Imekuwa mchezaji muhimu Libya, Palestina na Syria.
3. Nafasi ya TİKA katika diplomasia ya dini
TİKA imekuwa chombo muhimu katika kupanua ushawishi wa Uturuki:
- Inafanya kazi kama mkono wa nguvu laini.
- Ujenzi wa misikiti, ukarabati wa turathi za Ottoman, miradi ya misaada.
- Kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na mataifa ya Asia, Afrika na Ulaya.
Sehemu ya Tatu: Changamoto na Ukosoaji wa Ndani
Dkt. Khamehyar aligusia pia changamoto za mfumo wa AKP:
1. Lawama za “kuidhinisha dini kiserekali”
Serikali inadaiwa kutumia dini kama chombo cha kubaki madarakani.
2. Kupungua kwa demokrasia
Mfumo wa urais wenye nguvu umepunguza usimamizi wa bunge, jambo linaloleta wasiwasi kwa vyama pinzani.
3. Kuongezeka kwa mgawanyiko wa kijamii
- Mgawanyiko kati ya wasekula na Waislamu.
- Mgawanyiko wa kikabila (Waturuki/Kurdi).
- Mgawanyiko kati ya Alevi na Sunni, ambapo Alevi wanalalamikia upendeleo wa Sunni.
Dkt. Khamehyar alieleza kuwa Uislamu wa kisiasa nchini Uturuki umebadilika kutoka mfumo wa kiliberali wa miaka ya 1990 kwenda katika mfumo wa usalama, utaifa na utambulisho.
Taasisi ya Diyanet (Ofisi ya Mambo ya Dini) sasa imekuwa chombo muhimu katika siasa na diplomasia ya Uturuki, hasa baada ya jaribio la mapinduzi la 2016.
Sehemu ya Nne: Uchambuzi wa Mustakabali wa Uislamu wa Kisiasa Uturuki
Dkt. Khamehyar alisema mustakabali wa Uislamu wa kisiasa nchini Uturuki unategemea mambo matatu:
- Miundo iliyojengwa katika kipindi cha miaka 20 ya utawala wa AKP
- Mabadiliko ya kijamii yaliyojengeka
- Tabia ya kisiasa ya kizazi kipya
Alieleza senari 4 za mustakabali:
- Kupungua kwa nguvu ya AKP
- Kuongezeka kwa ushawishi wa wasekula
- Kuongezeka kwa nafasi ya jamii za kidini
- Kupungua kwa Uislamu wa kisiasa wa vyama na kuongezeka kwa Uislamu wa kijamii
Hitimisho la Dkt. Khamehyar
“Kwa mtazamo wangu, Uturuki ya baadae haitakwenda katika Uislamu wa kisiasa wa kiwango cha juu kabisa, wala haitarudi kwenye kisekula cha zamani. Uturuki itajenga utambulisho mpya wa kidini wa Kituruki. Kudumu kwa chama cha AKP kwa miaka 20 kumeubadilisha Uislamu wa kisiasa milele. Ushindani kati ya Waislamu wa kisiasa na wasekula utaendelea.”