4 Julai 2026 - 22:09
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Njia ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu itaendelea kwa nguvu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei (Quds Sirruh), si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya kuendeleza hadhi ya Uislamu na Iran, huku njia na misingi yake ikiendelea kwa nguvu na uthabiti.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa leo Jumamosi kwa mnasaba wa kuuaga mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah al-Udhma Imam Sayyid Ali Khamenei (Quds Sirruh), ikisisitiza kwamba njia na fikra za kiongozi huyo zitaendelea kwa nguvu na azma kubwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa wananchi wa Iran, kwa huzuni kubwa, wanaomboleza kuondokewa na Imamu na Kiongozi wao mwenye hekima, lakini wamegeuza tukio hilo la kihistoria kuwa fursa ya kuhuisha upya ahadi yao kwa misingi yake ya juu, pamoja na kulinda mafanikio ya uhuru, heshima na nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wizara hiyo pia imetoa salamu za rambirambi na pongezi kwa mrithi wa Kiongozi Shahidi, Ayatollah Sayyid Mujtaba al-Husseini al-Khamenei (Mwenyezi Mungu amhifadhi), kwa wananchi wa Iran, Marjaa wakuu wa dini, wanazuoni wa Kiislamu, Umma wa Kiislamu na watu wote huru duniani.

Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa Kiongozi Shahidi aliongoza Iran katika siasa za ndani na za nje kwa kuzingatia kauli ya Mwenyezi Mungu:
“Basi Mwenyezi Mungu ataleta watu anaowapenda na wao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu dhidi ya makafiri, wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu wala hawaogopi lawama za mwenye kulaumu…” (Al-Maidah: 54).

Wizara hiyo imeongeza kuwa msimamo, uthabiti na kujitolea kwa Kiongozi Shahidi katika njia ya haki, uadilifu na ubinadamu havikuwa tu sababu ya heshima na nguvu ya Iran, bali pia viligeuka kuwa chanzo cha msukumo kwa mataifa na watu huru duniani.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa ushiriki mpana wa makundi mbalimbali ya kidini na kitaifa kutoka eneo la Mashariki ya Kati pamoja na wajumbe rasmi wa ngazi za juu kutoka mataifa mbalimbali katika shughuli za kuuaga mwili wa Kiongozi Shahidi, ni ishara ya wazi ya hadhi na nafasi kubwa aliyokuwa nayo pamoja na heshima ya taifa la Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje imewashukuru wageni wote wa kigeni ambao, licha ya vitisho na mashinikizo, walishiriki katika shughuli hizo na kusimama upande wa haki na ukweli.

Mwisho, taarifa hiyo imesisitiza kuwa kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi si mwisho wa njia, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya kuendeleza hadhi ya Uislamu na Iran, na kwamba wananchi wa Iran, chini ya uongozi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wataendelea kuhifadhi jina, urithi na njia ya Kiongozi Shahidi kwa heshima na nguvu, huku wakifuatilia kwa dhati utekelezaji wa haki dhidi ya wahalifu wa Marekani na utawala wa Kizayuni.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha