Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) – ABNA – Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araghchi, amepongeza misimamo ya thamani ya Jamhuri ya Congo katika majukwaa ya kimataifa ya kuunga mkono Iran.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa mkutano kati ya Araghchi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kongo, Constant Serge Bonda, ambaye alifika mjini Tehran kushiriki katika marasimu ya kuuaga mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei (Quds Sirruh).
Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo aliwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kongo, serikali na wananchi wa nchi hiyo, akieleza mshikamano wao na serikali pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha, alimpa pole Iran kufuatia kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na viongozi wengine na wananchi wa Iran waliouawa katika kile alichokitaja kuwa ni uvamizi wa pamoja wa utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa upande wake, Araghchi alisisitiza kuthamini msimamo wa Kongo katika kuunga mkono Iran kwenye medani za kimataifa na kueleza matumaini ya kuimarishwa zaidi kwa uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Your Comment