19 Januari 2015 - 20:10
 Mapigano yongezeka nchini Yemen

Waasi wa Huthi nchini Yemen wamepambana vikali hii leo na wanajeshi karibu na ikulu ya Rais katika mji mkuu Sanaa

Waasi wa Huthi nchini Yemen wamepambana vikali hii leo na wanajeshi karibu na ikulu ya Rais katika mji mkuu Sanaa, na kulitumbukiza zaidi taifa hilo katika msukosuko wa kisiasa huku waasi hao wakishutumiwa kwa kujaribu kuipindua serikali. Miripuko imesikika mjini humo na moshi mkubwa kufuka huku waasi hao wakikidhibiti kituo cha habari cha serikali. Maafisa wa afya wamesema kiasi ya watu watano wameuawa na wengine karibu ishirini kujeruhiwa katika mapambano hayo huku idadi ya waathiriwa ikitarajiwa kupanda. Waziri wa habari nchini Yemen Nadia al Saqqaf amesema makaazi ya rais yameshambuliwa moja kwa moja katika kile kinachochukuliwa kuwa jaribio la mapinduzi. Jumuiya ya nchi za kiarabu imezitaka pande zote mbili zinazozozana kusitisha mara moja mapigano na kuiheshimu serikali iliyoko madarakani.

 

 

Lebo