(ABNA24.com) Hivi sasa tuko katika siku za mwisho za mwezi wa 52 wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Vita hivyo vina pande tofauti ambapo mojawapo ni kadhia ya uchumi. Kwa mujibu wa ripoti za asasi za kimataifa, moja ya athari za vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu, ni kuharibiwa asilimia 80 ya miundombinu ya Yemen. Itafahamika kuwa, mwishoni mwa mwaka wa nne wa vita hivyo vya Saudia nchini Yemen, mtandao wa habari wa Khaleej Online ulitangaza kwamba kwa mujibu wa taarifa rasmi kuhusu Yemen, inatazamiwa kuwa gharama ya ukarabati wa nchi hiyo utafikia karibu Dola bilioni 100. Zaidi ya hayo ni kwamba, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetoa taarifa mpya ambayo ilichapishwa mwezi Mei mwaka huu ikisema kuwa: "Raia milioni 24 wa Yemen, yaani asilimia 80 ya jamii inayojumuisha pia watoto zaidi ya milioni 12, wanahitaji misaada zaidi ya kibinaadamu suala ambalo limeufanya mgogoro wa Yemen kuwa mkubwa zaidi duniani kutokana na hali mbaya ya kibinaadamu. Sambamba na ripoti hiyo, watu milioni 19.7 wanahitaji uangalizi wa kiafya, huku zaidi ya watoto laki tatu na elfu 60 walio chini ya umri wa miaka mitano, wakiwa wanakabiliwa pia na hali mbaya ya utapiamlo."
Hii ni sehemu ndogo tu ya hasara za vita iliyogharimu kwa akali Dola bilioni 100 za Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Pamoja na hayo Abdallah al-Mouallimi, mwakilishi wa Saudia katika Umoja wa Mataifa amedai kwamba serikali ya Riyadh ni moja ya nchi ambazo zimekuwa zikishiriki katika njia ya kutoa misaada ya kibinaadamu kwa Yemen ambapo mwaka huu pekee imetoa zaidi ya Dola milioni 400. Mataimshi hayo ya Abdallah al-Mouallimi ni yenye nukta kadhaa muhimu zinapasa kuchunguzwa. Kwanza ni kwamba, mwakilishi huyo wa Saudia katika Umoja wa Mataifa anajaribu kupotosha fikra za waliowengi kuhusiana na jinai za Riyadh ilizozitenda nchini Yemen kwa kuwa kiasi cha Dola milioni 400 alizozitaja ni kiasi kidogo sana kwa ajili ya kufidia mgogoro mkubwa wa kibinaadamu ambao umesababishwa na Saudia ndani ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Pili ni kwamba, hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa kiasi hicho cha Dola milioni 400 za Saudia, ambazo bado zinatiliwa shaka, zilikabidhiwa raia wa Yemen wanaohitajia misaada ya dharura ya kibinaadamu.
Hii ni kusema kuwa misaada hiyo ya kimaonyesho ilikabidhiwa kwa vibaraka tu wa Riyadh. Nukta ya tatu ni kwamba hata kama Saudia mwaka huu itakuwa imetoa kiasi hicho cha Dola milioni 400 kwa ajili ya misaada ya kibinaadamu nchini Yemen, yote hayo ni kwa ajili tu ya kuzihadaa fikra za walio wengi duniani, kwa kuwa nchi ambayo mashambulizi yake ya kila siku yameibua mgogoro mkubwa zaidi wa kibinaadamu duniani, haiwezi kuwa ni 'nchi inayopenda vita' na wakati huo huo kuwa 'nchi mfadhili.' Kwani ufadhili na kupenda vita ni mambo mawili yanayopingana wazi na ambayo hayathibiti kwa nchi moja. Na nukta ya mwisho ni kwamba, Saudia imeisababishia Yemen ambayo ni nchi masikini zaidi ya Kiarabu eneo la Asia Magharibi hasara ambayo kwa uchache ni kiasi cha Dola bilioni 100 ambapo katika kipindi cha miezi 52 iliyopita si tu kwamba haikuweza kupata athari yoyote ya ushindi katika vita hivyo, bali ni kwamba athari za kushindwa utawala wa Aal Saud katika vita hivyo zinazidi kuonekana wazi siku hadi siku.
/129
20 Julai 2019 - 07:48
Msimbo wa Habari: 962815
Utawala wa Aal-Saud unadai kwamba ni serikali kubwa zaidi inayotoa misaada kwa Yemen, katika hali ambayo hadi sasa Yemen inashuhudia maafa makuba ya kibinaadamu kutokana na athari ya jinai zinazotekelezwa na utawala huo dhidi yake.