Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - Katika makala hii tutazungumzia umuhimu wa Qur’an Tukufu katika Maisha ya Wanadamu. Ndugu msomaji, Amani ya Mwenyeezi Mungu iwe juu yako na karibu sana katika somo murwa kabisa kuhusiana na umuhimu wa Qur’an Tukufu.
Ni jambo lisilokuwa na shaka ndani yake kuwa Qur’an hii Tukufu ni ahadi ya Mwenyeezi Mungu (s.w) ambayo imemuwezesha mwadanamu kutengeneza dini yake na dunia yake na kudhamini mafanikio ya akhera yake.
Na kila Aya katika Aya za Qur’an ni chimbuko la mwangaza, muongozo na rahma, kwa hiyo mwenye kutaka mafanikio ya milele na kuokoka katika dunia yake, basi ni juu yake kushikamana na kitabu cha Mwenyeezi Mungu (s.w) usiku na mchana na kuzifanya Aya za Qur’an Tukufu kuwa mfano katika kumbukumbu zake na kituo cha fikra zake ili awe katika mwangaza wa Mwenyeezi Mungu (s.w).
Amesema Imam Ali (a.s): “Someni Qur’an kwani Qur’an ni hadithi nzuri, na izingatieni hakika yake ni mlezi wa nyoyo, jitibuni kwa nuru yake, hakika ni ponyo la vifua, na isomeni vizuri hakika ni visa vyenye manufaa….” (Nahjal – Balagha: Hotuba ya 110).
- Fadhila za kusoma Qur’an Tukufu
Amesema Mtume Muhammad (s.a.w.w):”Mwenye kusoma Aya kumi kila usiku hatakuwa katika watu walio ghafilika, na mwenye kusoma Aya hamsini ataandikwa kuwa ni katika watu wenye kumbukumbu, na mwenye kusoma Aya mia moja ataandikwa kuwa ni katika watu wamchao Mwenyeezi Mungu (s.w),na mwenye kusoma Aya mia mbili ataandikwa kuwa ni katika watu wenye kumnyenyekea, na mwenye kusoma Aya mia tatu , ataandikwa kuwa ni katika watu ambao wamefuzu, na Mwenye kusoma Aya mia tano ataandikwa kuwa ni katika watu wenye kujitahidi….”.Rerea: (Al-Bayan:Uk wa 25).
- Adabu za kusoma Qur’an Tukufu.
Kwa kuwa Qur’an ni Kitabu chenye heshima ya juu na daraja kubwa na utukufu wa hali ya juu, hakuna shaka kwamba kuisoma kwake kunataratibu na adabu zake ambazo ni lazima kuzichunga kwa kila mwenye kutaka kusoma Qur’an.Na adabu zenyewe zimegawanyika sehemu tatu:-
- Adabu kabla ya kuanza kuisoma Qur’an.
- Adabu wakati unaisoma Qur’an.
- Adabu baada ya kuisoma Qur’an.
- Adabu kabla ya kuanza kuisoma Qur’an.
- Twahara. Ni sunna kwa mwenye kuisoma Qur’an awe na tohara ya hadathi ndogo na hadathi kubwa kama ilivyopokelewa kutoka kwa Imam Ali (a.s) amesema: “Mja wa Mwenyeezi Mungu (s.w) asisome Qur’an kama (atakuwa) hana udhu mpaka achukue udhu”. Rejea: (Wasailu-Shia: Juzuu ya 2. Ukurasa wa 847). Ama kuhusu kuyagusa maandishi ya Qur’an Tukufu pia ni haramu kwa mtu ambaye hana tohara ya hadathi kubwa na ndogo kuyagusa maandishi hayo ya Qur’an Tukufu kama alivyo sema Mwenyeezi Mungu (s.w). “Haigusi hii Qur’an ila mwenye tohara”. (56:79). Ama kuibeba Qur’an bila kugusa Aya zake ni makuruhu kwa mtu mwenye hadathi kubwa.
- Mswaki. Ni sunna kwa mwenye kutaka kusoma Qur’an.
Kupiga mswaki kama ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume Muhamad (s.a.w.w): “Safisheni njia ya Qur’an, akaulizwa Mtume: Ewe Mtu wa Mwenyeezi Mungu (s.w) ni ipi hiyo njia ya Qur’an?. Akasema Mtume (s.a.w.w):Vinywa vyenu.” Akaulizwa tusafisheje?. Akasema Mtume (s.a.w.w:) Kwa kupiga mswaki.
Rejea:(Biharul – An’wari:Juzuu ya 76.Ukurasa wa 131).
- Kujikinga. Inatakiwa kwa mwenye kutaka kuisoma Qur’an, aanze kwa kujikinga kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) kutokana na shetani aliyelaaniwa, kama anavyosema Mwenyeezi Mungu Mtukufu.
“Na ukitaka kuisoma Qur’an basi jikinge kwa Mwenyeezi Mungu -(s.w)- akulinde na shetani aliyelaaniwa”. (16 : 97).
- Dua. Na katika dua ambazo zimependekezwa zaidi kabla ya kusoma Qur’an Tukufu ni dua hii ifuatayyo:- “Ewe Mwenyeezi Mungu wa haki niongezee mapenzi zaidi katika hii Qur’an, uijalie iwe nuru ya macho yangu na ponyo ya kifua changu na iweze kuondoa shida zangu, matatizo na huzuni yangu, Ewe Mwenyeezi Mungu wa haki ifanye Qur’an ni yenye kuupamba ulimi wangu na kung’arisha uso wangu kwa Qur’an na mwili wangu uwe na nguvu, na kipimo (mizani) changu kiwe kizito na uniwezeshe nisome Qur’an kwa ajili ya kukutii wewe usiku na mchana na unifufue nikiwa pamoja na Muhammad na Kizazi chake bora na chema”.
ii. Adabu wakati inasomwa Qur’an Tukufu.
- Kuziangalia Aya.
Ni sunna kwa mwenye kusoma Qur’an Tukufu awe anaiangalia badala ya kuisoma kwa kuhifadhi kama alivyosema Mtume Muhamad (s.a.w.w): “Ibada bora juu ya umati wangu ni kuisoma Qur’an Tukufu kwa kuiangalia”. Rejea:(Usulul_Kafi: Katika Mlango wa fadhila za Qur’an).
- Kunyenyekea. Ni sunna kwa mwenye kusoma Qur’an awe mnyenyekevu na ajiepushe na kucheka hovyo na kufanya mzaha na kukata maneno ya Qur’an na kuongea na watu wengine, na ni makuruhu kula na kutembea huku unasoma Qur’an.
(c) Kuzingatia. Ni juu ya msomaji wa Qur’an kufanya mazingatio wakati anasoma Aya za Qur’an kama alivyo sema Mwenyezi Mungu: “Je, hawaizingatii Qur’an au nyoyo zinakufuli”?.(47: 24).
(d) Kusujudu. Ni lazima kusujudu wakati utakapo soma au kusikia Aya hizi Tukufu
zikisomwa katika sura hizi ambazo zinaitwa Suratul-Azaaimu ambazo ni nne:-
(1)-Surat Sajdah (32): 15, (2)-Surat Fuswilat / Haamiim Saidah (41):38, (3)-Surat Najmu (53):62 na (4)- Surat Alaq (96):19, ama Aya nyingine kumi zilizo kwenye sura nyingine zisizo kuwa hizi ukizisoma au kusikia zinasomwa kusujudu ni sunna. Ndani ya Qur’an kuna Aya za sajda kumi na nne (14) kumi ni za suna na nne ni za wajibu.
iii. Adabu baada ya kusoma Qur’an.
- Ni sunna kwa mwenye kusoma Qur’an atakapo maliza kusoma Qur’an Tukufu asome Suratul- Fatiha na Aya tano za mwanzo katika Surat Baqara.
- Kusoma dua zilizo pendekezwa na katika hizo ni :-
“Amesema kweli Mwenyeezi Mungu Mtukufu na aliyetukuka na akasema kweli na kufikisha Mtume wake mwaminifu na mkarimu na sisi juu ya hilo ni wenye kushuhudia na wenye kushukuru na amani iwe juu ya Mitume waliotumwa na sifa njema anastahiki Mwenyeezi Mungu (s.w) Mola wa ulimwengu”.
- Mazingatio ndani ya Qur’an Tukufu.
Hakika Qur’an ni Kitabu ambacho amekiteremsha Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa mpangilio, watu wanaongoka kwa kutumia kitabu hicho katika dunia yao na nuru yake inawaangazia katika njia zao nyingine. Mafanikio haya hayapatikani isipokuwa kwa kuzingatia na kutafakari katika maana yake.
Imepokewa misisitizo mingi ndani ya Qur’an Tukufu yenyewe na katika Sunna za Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) juu ya kuisoma vizuri Qur’an Tukufu na kuizingatia au kwa ibara nyingine tunaweza kusema: Kutafakari juu ya makusudio yake na malengo yake.Anasema Mwenyeezi Mungu (s.w): Je,hawazingatii hii Qur’an au nyoyo zimekufa?. (47:24).
Imam Ali bin Abi Talib (a.s) naye amesema: “Qur’an inatoa nasaha bila kughushi, na muongozo usiopotea, ni mzungumzaji ambaye hadanganyi, hakuikalisha Qur’an mtu yeyote ispokuwa ataondoka na nyongeza au upungufu. Tambua kwamba hakuna kitu chochote ambacho kiko juu ya Qur’an wala chenye kujitosheleza kama Qur’an, basi itumieni kutibu maradhi yenu na jikingeni kwa Qur’an matatizo yenu kwani ndani ya Qur’an kuna ponyo ya maradhi makubwa nayo ni ukafiri, unafiki, chuki, upotevu, hivyo muombeni Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa kutumia Qur’an na muelekeeni Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa kutumia Qur’an, na kwa kuipenda, na msiwaombe viumbe kwa kutumia Qur’an kwa sababu hakuna kitu kinachoweza kuwaelekeza waja kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) zaidi ya Qur’an kwani atanadi mwenye kunadi siku ya mwisho, kwamba: Tambueni kuwa kila aliyepanda atapimwa kwa alichokipanda mwisho wa maisha yake ispokuwa aliyepanda Qur’an huyo hataulizwa, hivyo ipendeni Qur’an na kuifuata na itumieni kuwa dalili juu ya Mola wenu, itumieni kunasihi nafsi zenu na acheni maovu na matamanio yenu juu ya Qur’an”. Rejea ndani ya:(Nahjul- Balagha: Hotuba ya 176).
Hadithi nyingi sana zipo zinazo wahimiza waislam kuwa na mazingatio katika Aya za Qur’an lakini kwa leo tutosheke na hizi tulizozitaja.
Wabillah Taufiq.
Makala hii imeandaliwa na: Sheikh Idrissa Ibrahimu.
Your Comment