Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mashirika nane ya kiusalama na maafisa wa Marekani wametoa tathmini kwamba mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran hayakufanikisha kuangamiza mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, bali yalichelewesha tu kwa muda wa miezi michache. Iran bado ina uwezo wa kuendeleza shughuli za kurutubisha urani na hata kutengeneza silaha za nyuklia iwapo itaamua.
Zifuatazo ni tathmini 8 za Mashirika ya Kijasusi ya Marekani kuhusu kufeli na kushindwa kwa Trump katika Shambulizi lake dhidi ya Miundo Mbinu ya Nyuklia ya Iran:
1. Tathmini Mpya ya Kijasusi ya Marekani
NBC News iliripoti kuwa mashambulizi ya anga ya Marekani yaliharibu kituo kimoja tu kati ya vitatu vya nyuklia.
Rais wa zamani Trump alikataa mpango wa mashambulizi ya kina ambayo yangechukua wiki kadhaa, kutokana na hofu ya vita vikubwa na vifo vingi.
Tathmini inaonyesha kwamba Iran inaweza kuanza tena urutubishaji urani ndani ya miezi michache.
2. Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Zamani – Jake Sullivan
Sullivan alisema:
“Mashambulizi hayakuleta matokeo yaliyotarajiwa. Suluhisho bora lingekuwa makubaliano ya kudhibiti uwezo wa nyuklia wa Iran kwa muda mrefu.”
3. Shirika la Ujasusi la Ulinzi (DIA)
Taarifa ya DIA ilieleza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ulicheleweshwa kwa miezi 3 hadi 6 pekee.
Pia, walibainisha kuwa Iran ina mitaro ya ardhini isiyopenyeka hata kwa mabomu mazito aina ya GBU-57.
4. Waziri wa Mambo ya Nje – Antony Blinken
Blinken alisema:
“Kabla ya shambulizi, Iran haikuwa na nia ya kutengeneza bomu. Lakini sasa, kuna hatari kuwa inaweza kuamua kulifanya mpango wake kuwa wa kijeshi.”
5. Tathmini ya CENTCOM (Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani)
CENTCOM ilieleza kuwa sehemu muhimu za mpango wa nyuklia hazikuangamizwa bali zimecheleweshwa tu kwa muda mfupi.
6. Ripoti ya New York Times
Ripoti ilisema kuwa mashambulizi ya Marekani yalifunga milango ya kuingilia tu, lakini mahandaki ya chini ya ardhi hayakuathirika.
7. Washington Post na Operesheni “Midnight Hammer”
Ripoti ilieleza kuwa kituo viwili vya nyuklia havikuangamizwa na taarifa za ndani zinatahadharisha kuwa madai ya kufanikisha uharibifu kamili yalikuwa ya kupotosha.
8. Maseneta wa Marekani
Baada ya kikao cha ndani cha maafisa wa utawala wa Trump na maseneta, baadhi ya maseneta walipinga madai ya Trump.
Seneta Chris Murphy alisema:
“Inaonekana tulichelewesha tu mpango wa Iran kwa miezi michache. Madai ya kuuangamiza kabisa ni ya uongo.”
Kwa ujumla:
Tathmini nyingi kutoka ndani ya vyombo vya usalama vya Marekani zinaonyesha kuwa Iran bado ina uwezo wa kuendeleza mpango wake wa nyuklia. Badala ya kuuzuia, mashambulizi ya Marekani huenda yameifanya Iran kuwa na msimamo mkali zaidi na kufikiria kuujenga kwa matumizi ya kijeshi.
Your Comment