Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- chanzo hicho kilisema kuwa vikosi vya muungano wa kimataifa vitaondoka katika kambi ya Ain al-Asad, uwanja wa ndege wa Baghdad na makao makuu ya operesheni za pamoja, na kuhamishiwa Erbil.
Chanzo hicho kilifafanua kuwa mchakato huu wa kuondoka utafanyika mwezi Septemba kwa mujibu wa makubaliano kati ya Baghdad na Washington. Aidha, walimu na wakufunzi wa kijeshi wa Marekani wataendelea kubakia nchini Iraq, na uwepo wao hautahusiana na kuondoka kwa vikosi vya muungano.
Taarifa ya Al-Sumaria News pia imekumbusha kuwa tayari kumekuwepo na ripoti kuhusu kuanza kuhamishwa kwa vifaa vya kijeshi vya Marekani kutoka kambi ya Ain al-Asad iliyoko magharibi mwa Iraq. Hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano ya Baghdad na Washington ya kumaliza rasmi jukumu la kijeshi la muungano wa kimataifa. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya Marekani kufikia Septemba 2026 vitabaki tu Erbil na maeneo ya kaskazini mwa Iraq.
Ikumbukwe kuwa tangu Januari 2024, kamati ya pamoja ya kijeshi kati ya Iraq na muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani iliundwa kwa lengo la kupitia upya jukumu la muungano huo katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).
Katika taarifa ya ofisi ya habari ya Waziri Mkuu wa Iraq iliyotolewa wakati huo, ilisisitizwa kuwa kumalizika kwa jukumu la kijeshi la muungano wa kimataifa dhidi ya Daesh baada ya kupita miaka kumi tangu kuanzishwa kwake na baada ya mafanikio makubwa kupatikana, jukumu la ufuatiliaji na usimamizi litabaki mikononi mwa wataalamu wa kijeshi wa Iraq.
Your Comment