1 Septemba 2025 - 23:38
Ujerumani Yapokea Kundi la Kwanza la Wakimbizi wa Kiafghan Baada ya Miaka Mitatu ya Kusubiri

Baada ya miezi kadhaa ya kusubiri na shinikizo kutoka kwa mahakama, Ujerumani hatimaye imepokea kundi la kwanza la wakimbizi wa Afghanistan waliokimbia utawala wa Taliban.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, watu 46 kutoka Afghanistan waliokuwa wamekwama nchini Pakistan waliwasili leo Jumatatu nchini Ujerumani, baada ya uamuzi wa mahakama uliolazimisha Serikali ya Ujerumani kuwapa hifadhi.

Ndege iliyowabeba ilitokea Istanbul, Uturuki na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Hanover majira ya saa 6 mchana. Kundi hilo lilijumuisha familia 10 za Kiafghan, na lililetwa kupitia juhudi za shirika lisilo la kiserikali linaloitwa "Daraja la Anga la Kabul" (Kabul Air Bridge). Mtu wa 47 wa kundi hilo hakufanikiwa kuunganisha safari yake kutoka Istanbul lakini anatarajiwa kuwasili baadaye leo.

Hiki ndicho kikundi cha kwanza cha wakimbizi wa Afghanistan kilichopokelewa na Ujerumani tangu serikali mpya chini ya Kansela Friedrich Merz ilipoingia madarakani mwezi Mei.

Awali, muungano wa serikali unaojumuisha wahafidhina na chama cha Social Democrats ulikuwa umesimamisha kwa kiasi kikubwa mpango wa kuwapokea wakimbizi wa Afghanistan, kama sehemu ya sera kali za uhamiaji zilizochochewa na ongezeko la ushawishi wa chama cha mrengo wa kulia cha AfD – "Alternatif für Deutschland".
Hata hivyo, mahakama za Ujerumani ziliilazimisha serikali kutekeleza ahadi zake za awali kuhusu wakimbizi hawa.

Wakati huo huo, hali ya wakimbizi wa Afghanistan walioko Pakistan inaendelea kuwa mbaya, huku serikali ya Islamabad ikianza operesheni ya kuwafukuza kwa nguvu tangu mwezi Aprili. Serikali ya Ujerumani wiki iliyopita ilitangaza kuwa itaruhusu baadhi ya wakimbizi hao kuingia nchini humo.

Eva Bayer, msemaji wa mpango wa "Daraja la Anga la Kabul", alisema kuwa watu hao walikuwa wanasubiri hifadhi ya Ujerumani kwa muda wa takribani miaka mitatu. Alieleza kuwa watu 10 kati yao — akiwemo wanawake wanane na wanaume wawili — walikuwa ni wanaharakati wa kisiasa, waandishi wa habari, na watetezi wa haki, huku mmoja wao akiwa daktari aliyehudumu katika jeshi la Ujerumani.

Kwa sasa, zaidi ya raia 2,100 wa Afghanistan walioahidiwa hifadhi na Ujerumani bado wako Pakistan wakiwa katika hali ya sintofahamu. Aidha, takribani watu 200 tayari wamelazimishwa kurejea Afghanistan na serikali ya Pakistan.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani alisema kuwa mchakato wa kuchakata maombi ya wakimbizi unaweza kuchukua muda, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ikisisitiza kuwa Berlin inaendelea kufanya kazi kuhakikisha wanaendelea kuwapokea walioahidiwa hifadhi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha