Kwa mujibu wa shirika la habari la AhlulBayt (ABNA), azimio hilo limeungwa mkono na asilimia 86 ya wanachama waliopiga kura, kati ya wanachama 500 wa Chama cha Kimataifa cha Wataalamu wa Utafiti wa Mauaji ya Kimbari.
Azimio hilo linaeleza kuwa sera na vitendo vya Israel katika Gaza vinaendana na tafsiri ya kisheria ya mauaji ya kimbari iliyobainishwa katika Kifungu cha Pili cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948.
Ripoti ya chama hicho inaeleza kuwa tangu tarehe 7 Oktoba 2023, serikali ya Israel imehusika katika mfululizo wa uhalifu mkubwa na wa mpangilio dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, na mauaji ya kimbari. Vitendo hivi vinajumuisha mashambulizi yasiyo na mwelekeo kwa raia na miundombinu ya kiraia kama vile hospitali, nyumba, majengo ya biashara, na taasisi nyingine, pamoja na mateso na kunyimwa chakula na maji.
Ripoti hiyo pia inasisitiza kuwa jeshi la Israel limewaua au kuwajeruhi zaidi ya watoto 50,000 — jambo linalotajwa kuwa moja ya viashiria vya mauaji ya kimbari kwani linahatarisha uwepo wa kundi la watu kwa ujumla. Aidha, mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu, wafanyakazi wa afya, na waandishi wa habari pia yametajwa kuwa sehemu ya uhalifu huo.
Kulingana na ripoti hiyo, hatua zilizochukuliwa na Israel kama jibu kwa shambulio la tarehe 7 Oktoba hazikulenga tu kundi la Hamas, bali zililenga wakaazi wote wa Gaza.
Chama hicho kimetahadharisha kuwa jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, ili kuzuia kutokea kwa jinai hiyo.
Mwisho wa ripoti hiyo unasema kuwa hatua zinazodaiwa kuwa za kiusalama dhidi ya wanachama wa kundi fulani - kwa maana ya kile ambacho Israel inakiita operesheni dhidi ya Hamas - mara nyingi hutumika kama kisingizio cha mauaji ya halaiki na mauaji ya kimbari ya watu wengi.
Your Comment