Kwa mujibu wa shirika la habari la AhlulBayt (a.s) -ABNA- Kundi la kigaidi la ISIS tawi la Pakistan limetoa taarifa rasmi likidai kuhusika na shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililotokea usiku wa kuamkia leo katika mji wa Quetta, makao makuu ya Jimbo la Balochistan, nchini Pakistan.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya "Khorasan Diary", ISIS ilimtaja Ali al-Muhajir kuwa ndiye mshambuliaji wa kujitoa mhanga na pia ilichapisha picha yake katika taarifa hiyo.
Shambulio hilo lilitokea karibu na Uwanja wa Shahwani, wakati wa mkutano wa kisiasa wa chama cha Balochistan National Party (BNP). Kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo, angalau watu 13 waliuawa na wengine 30 kujeruhiwa katika mlipuko huo.
Tukio hili limezidisha hofu kuhusu kuenea kwa shughuli za makundi ya kigaidi katika eneo la mpaka kati ya Afghanistan na Pakistan.
Mwakilishi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa, Asim Iftikhar, hivi karibuni alitoa onya kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa kundi la ISIS-Khorasan ndani ya Afghanistan na uhusiano wake na makundi ya kigaidi yanayofanya mashambulizi ndani ya Pakistan.
Your Comment