22 Septemba 2025 - 18:21
Madai ya Ukinzani kati ya Fitra ya Upweke wa Mungu (Tawhidi) na Uwepo wa Ushirikina na Miungu Mingi

Chanzo: Kituo cha Kitaifa cha Majibu ya Maswali ya Dini | Swali: Ikiwa Binadamu wote wana Fitra moja ya kumpwekesha Mungu na Manabii (as) daima wamekuwa wakiwaita watu katika ibada ya Kumuabudi Mwenyezi Mungu Mmoja, basi kwa nini katika historia, jamii nyingi kama Waarian wa kale au Wahindu walipata kuangukia kwenye ushirikina na ibada ya miungu mingi? Je, jambo hili si kinzani na madai ya kidini (juu ya Fitra ya Mwanadamu kuwa ya kumpwekesha Mwenyezu Mungu)?.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Fitra, ingawa ni ya kimungu na imewekwa ndani ya nafsi ya mwanadamu, lakini kama ilivyo kwa uwezo mwingine wa kibinadamu, inahitaji malezi na uangalizi. Ikiwa itawekwa katika mazingira ya malezi mabaya au kupuuzwa, hupungua nguvu yake au hata mtu huanza kuikanusha.

Swali:
Ikiwa Binadamu wote wana Fitra moja ya kumpwekesha Mungu na Manabii (as) daima wamekuwa wakiwaita watu katika ibada ya Kumuabudi Mwenyezi Mungu Mmoja, basi kwa nini katika historia, jamii nyingi kama Waarian wa kale au Wahindu walipata kuangukia kwenye ushirikina na ibada ya miungu mingi? Je, jambo hili si kinzani na madai ya kidini (juu ya Fitra ya Mwanadamu kuwa ya kumpwekesha Mwenyezu Mungu)?


Nukta ya Kwanza: Fitra ni mwelekeo wa ndani, si kutimia kwa nje

Katika mtazamo wa Qur’ani, fitra ni asili na muundo wa ndani wa mwanadamu – mwelekeo wa kiasili wa kumtambua na kumwabudu kiumbe mkamilifu zaidi, yaani Mwenyezi Mungu. Hii ina maana kwamba mwelekeo wa tauhidi umewekwa ndani ya wanadamu, lakini si lazima kila wakati udhihirike kwa vitendo katika kila mtu au kila jamii.

Mfano:

  • Wema uko ndani ya fitra ya kila mtu, lakini historia imejaa wabaya.
  • Kutafuta ukweli ni sehemu ya fitra ya mwanadamu, lakini historia pia imejaa ujinga na ushirikina.
  • Haki ni tamaa ya wote, lakini dhuluma pia imeenea.

Kwa hiyo, fitra kama vipawa vingine vya mwanadamu, inahitaji mwongozo, ukuaji na uangalizi. Iwapo mtu hataki au hajalelewa vizuri na akakulia katika mazingira yenye ushirikina na upotovu, nuru ya fitra yake hudhoofika mpaka hata yeye mwenyewe haioni tena na anaweza kuikanusha.


Nukta ya Pili: Malezi ya Manabii na hiari ya watu

Ni kweli kuwa manabii ni walezi na waalimu wa kufundisha na kukuza fitra, lakini mpaka mtu na jamii iwe tayari kupokea mwongozo huo, mbegu ya ndani haitachanua. Qur’ani inasema: “Hakika Mwenyezi Mungu habadili hali ya watu mpaka wabadilike wenyewe yaliyo ndani ya nafsi zao.” (Qur’ani, Sura ar-Ra’d, Aya 11).

Mwanadamu si mmea kwamba akipata maji na mwanga automatically huchanua. Hapa, pamoja na mambo ya nje na ya ndani, ni lazima yeye mwenyewe pia atake. Hiari na ridhaa yake ndizo zinazoamulia.

Mfano: Wana wa Israeli waliona miujiza ya Nabii Musa na wakawa pamoja naye, lakini alipokawia kurudi kutoka Sinai, walivutwa na ndama wa Samiri na wakaangukia katika ushirikina. Musa aliporudi, wakatubu na kuacha ushirikina. Vivyo hivyo, historia ya dini za Kiajemi na Kihindi imekuwa na kwenda na kurudi kati ya tauhidi na ushirikina.


Nukta ya Tatu: Ushirikina kama upotoshaji wa tauhidi

Ushirikina si kuikanusha tauhidi kutoka asili, bali ni kupotosha na kupindisha mafundisho ya manabii na nuru ya fitra. Wengi wa washirikina walikuwa na imani kwamba Mungu yupo, lakini waliongeza miungu midogo kama washirika, wakidhani wanawakaribia kwa Mungu kupitia wao. Qur’ani inanukuu kauli yao: “Hatuwaabudu hawa ila kwa ajili ya kutukaribia kwa Mwenyezi Mungu.” (Qur’ani, Sura az-Zumar, Aya 3).

Kwa hiyo, hata katika jamii zenye ushirikina, nuru ya fitra haikuzimika kabisa; bali ilipotoshwa.


Nukta ya Nne: Sababu kuu za kuzuka kwa ushirikina

Qur’ani inataja sababu nyingi zinazowasukuma watu kuingia kwenye ushirikina, miongoni mwao:

  1. Kufuata mababu bila kufikiri“Wanaposemwa: fuateni aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, husema: bali tunafuata tuliyoyakuta kwa baba zetu.” (Qur’ani, Sura al-Baqara, Aya 170).

  2. Kufuata dhana na makisio“Ukiwatii wengi walioko duniani watakupoteza na njia ya Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana tu.” (Qur’ani, Sura al-An’am, Aya 116).

  3. Ujinga na kusingizia kwa Mungu“Watashirikina watasema: Lau Mwenyezi Mungu angalitaka tusingelishirikina sisi wala baba zetu.” (Qur’ani, Sura al-An’am, Aya 148).

  4. Kuzima akili na dhamiri“Wana nyoyo wasiofahamu, macho wasiyoona, masikio wasiyosikia. Hao ni kama wanyama bali ni wapotovu zaidi.” (Qur’ani, Sura al-A’raf, Aya 179).

  5. Kujivuna kwa mali na starehe za dunia“Hatukutuma mwonyaji katika mji wowote ila matajiri wake walisema: sisi tunakataa.” (Qur’ani, Sura Saba, Aya 34-35).


Hitimisho

Kwa hiyo, kuenea kwa ushirikina katika historia hakupingi fitra ya tauhidi. Kinyume chake, kunathibitisha kwamba bila malezi sahihi, ufuatiliaji wa manabii, na bidii ya binafsi, mwanadamu anaweza kupotoka kutoka katika nuru hiyo ya ndani.

Fitra ni nuru ya ndani ya mwanadamu, na manabii walitumwa kuhuisha na kuilinda. Kila mara jamii ilipowapinga manabii au kupotosha mafundisho yao, mazingira ya ushirikina yalijitokeza. Hivyo, imani ya fitra ya tauhidi na utume wa manabii si kinzani na historia, bali ndiyo ufafanuzi bora wa kwa nini mara nyingi watu walipotea kutoka njia ya tauhidi na walihitaji upya mwongozo wa kimungu.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha