Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naeem Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, leo Jumanne tarehe (7 Oktoba 2025) alituma ujumbe wa video kwa hafla ya kitaifa ya “Iran Hamdel” (Iran kwa moyo mmoja) iliyofanyika katika Hoseiniyya ya Imam Khomeini (r.a) mjini Tehran.
Katika ujumbe wake, Sheikh Qassem aliishukuru uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kiongozi wa Mapinduzi Imam Sayyid Ali Khamenei (h.a.), Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), taifa lenye juhudi na mashujaa wa Iran, na serikali ya Iran kwa msaada wao mkubwa kwa mstari wa mbele wa muqawama (mapambano), akisisitiza kuwa msaada huo umeifanya muqawama wa Lebanon kuwa na nguvu na azma isiyotetereka.
Sheikh Qassem alisema:
“Ninatoa bishara kwamba watoto wa Sayyid Hassan Nasrallah ni wapiganaji jasiri; familia za mashahidi na makamanda wote waliobaki imara katika njia ya kujitolea, kazi na maisha, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, wataendelea kuwa thabiti na watakataza Israel kufikia malengo yake. Kwa rehema za Mwenyezi Mungu, sisi tuko imara na wenye nguvu.”
Aliendelea kusema:
“Tunatoa shukrani za dhati kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khamenei (h.a), Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Sepah), taifa la Iran, serikali na vikosi vyake vya ulinzi, kwa sababu tumehisi kuwa Iran nzima - kutoka mwanzo hadi mwisho - imesimama pamoja nasi. Mmetupa nguvu, imani na ujasiri wa kupambana.”
Sheikh Qassem pia aliipongeza Iran ya Kiislamu kwa kusimama kwake kwa ushujaa mkubwa dhidi ya uvamizi wa Marekani na Israel kwa kipindi cha siku kumi na mbili, akisema:
“Alhamdulillah, mmeonyesha mfano kwa dunia nzima jinsi ya kupambana na uvamizi, kusimama imara, na kufikia mafanikio makubwa kwa baraka za uongozi wa Imam Khamenei (h.a), umoja wa watu na uaminifu wa wanajeshi wenu shupavu. Ushindi huu utaandikwa katika historia.”
Akaongeza kwa kusisitiza:
“Tunajua Iran inalipa gharama kubwa kwa kusimama upande wa haki, upande wa muqawama, upande wa Palestina, na upande wa mataifa yote yanayohitaji msaada. Lakini hii ndiyo Iran - mfano wa kujitolea, utukufu na uadilifu - ambayo haidai chochote kwa kusimama na wanyonge. Iran hii imesimama kwa ajili ya utukufu wa ubinadamu.”
Sheikh Qassem alizungumzia pia vikwazo vipya dhidi ya Iran, akisema:
“Leo tena wameiwekea Iran vikwazo vipya. Je, vikwazo hivi viliwahi kuacha kuwepo? Tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 46 iliyopita, Iran imeendelea kuwa chini ya vikwazo, lakini kila siku taifa hili limeendelea kung’aa zaidi na kuthibitisha kuwa ni taifa la ukweli na la mapambano.”
Na akahitimisha kwa aya tukufu:
“إن شاء الله nyinyi mtafaulu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu - ‘Na hakika ni jukumu letu kuwasaidia Waumini.’ (Surat Ar-Rum: 47).”
Your Comment