Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- katika moja ya usiku wa baridi kali mwezi Januari, Zahran Mamdani, mbunge wa jimbo ambaye hapo awali hakuwa maarufu sana, alivutia umakini wa umma baada ya kuchapisha video fupi akiwa kwenye mgahawa wa chakula cha halali Mjini Manhattan, New York - hatua iliyokuwa mwanzo wa nguvu yake ya kisiasa.
Miezi mitano baadaye, kupitia uongozi wenye mvuto, mtindo wa urahisi na ari ya kweli, pamoja na kampeni ya wananchi, aliweza kushinda nafasi ya kugombea Umeeya wa New York kupitia chama cha Demokratik, akiwapita wapinzani maarufu kama Andrew Cuomo.
Mkazo wake juu ya masuala yanayogusa maisha ya watu, ushirikiano na wanaharakati wa mageuzi, na matumizi bora ya mitandao ya kijamii uligeuza kampeni yake kuwa harakati ya kijamii iliyompa ushindi wa kushangaza - ushindi uliowashangaza hata wafuasi wake.
Zahran Mamdani, ambaye sasa ni mgombea rasmi wa chama cha Demokratik kwa nafasi ya Meya wa New York, amekuwa nembo ya kitaifa kutokana na kasi ya maendeleo yake kisiasa. Iwapo atashinda mwezi Novemba, atakuwa Meya wa kwanza Mwislamu wa jiji la New York - jambo ambalo limezua mijadala mikali na mashambulizi yasiyo na adabu kutoka kwa baadhi ya wanasiasa.
Wanasiasa wa mrengo wa kulia na viongozi wa mitaa wamemshambulia kwa lugha za matusi na ubaguzi wa rangi, wakijaribu kumharibia sifa. Andy Ogles, mbunge wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, alimuita kwa dhihaka “Little Muhammad” (Muhammad Mdogo) katika kitendo cha uchochezi wa chuki.
Nancy Mace, pia mbunge wa Republican, alimhusisha Mamdani na mashambulizi ya Septemba 11 kupitia mitandao ya kijamii.
Steve Bannon, mshauri wa zamani wa Donald Trump, na Laura Loomer, mwanaharakati wa mrengo wa kulia anayejulikana kwa kauli za chuki dhidi ya Uislamu, walimuita bila ushahidi “Mwislamu mwenye misimamo mikali.”
Mamdani tayari amewahi kutishiwa kuuawa na kukabiliwa na mashambulizi ya kisiasa, huku timu yake ikisisitiza kuwa vitendo hivyo ni ishara ya kuongezeka kwa chuki na Uislamu-fobia ambavyo havina nafasi katika jiji la New York.
Yeye na wafuasi wake wamesema hawataogopa chuki, ubaguzi wala vitisho.
Wapinzani wake wa kisiasa pia wamejaribu kumtuhumu kuwa mpinga Wayahudi kutokana na msimamo wake wa kukosoa utawala wa Kizayuni (Israel), ilhali Mamdani mara kadhaa amesisitiza kuwa anakataa aina zote za chuki dhidi ya Wayahudi, huku akisimamia haki za Wapalestina kwa njia zisizo za vurugu.
Licha ya mashambulizi hayo, jamii ya Kiislamu na wafuasi wengi wa ndani wanaonyesha matumaini makubwa kwa kuongezeka kwa umaarufu wa Mamdani.
Baada ya kuondoka kwa Meya wa sasa Eric Adams, kinyang’anyiro kimebaki na wagombea watatu wakuu, na tafiti za maoni zinaonyesha kuwa Andrew Cuomo anakabiliwa na changamoto kubwa, huku Mamdani akipata uungwaji mkono muhimu, ikiwa ni pamoja na idhini rasmi kutoka kwa Gavana wa New York.
Andrew Cuomo, ambaye alijiuzulu miaka minne iliyopita baada ya kuthibitishwa kuhusika katika unyanyasaji wa kingono wa wanawake 11, sasa amekuwa mwenye tahadhari zaidi hadharani, ingawa wapinzani kadhaa bado hawamchukulii kama mtu anayestahili nafasi ya Meya wa New York.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa awali wa chama cha Demokratik, Cuomo ametangaza kuwa ataendelea kugombea kama mgombea huru.
Curtis Sliwa, anayejulikana kwa kuanzisha kikundi cha “Guardian Angels” na upendo wake kwa paka, anaonekana kuwa na nafasi ndogo sana ya kushinda katika uchaguzi wa mwisho.
Your Comment