20 Oktoba 2025 - 17:47
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu:“Wazayuni hawakutarajia nguvu ya makombora ya Iran / Marekani haina haki kujihusisha na teknolojia ya Iran"

Ayatollah Sayyid Ali Khamenei amebainisha kwamba: Marekani haina haki kujihusisha na suala la teknolojia ya nyuklia ya Iran - na akahoji kuhusiana na Trump akisema: Wewe ni nani hasa?”.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa Wazayuni hawakutarajia kiwango kikubwa cha uharibifu uliosababishwa na makombora ya Iran katika vita vya siku 12, na akasisitiza kuwa Marekani haina mamlaka yoyote kuingilia masuala ya ndani ya Iran, ikiwemo sekta ya nyuklia.

Katika hotuba yake mbele ya mamia ya wanamichezo mashujaa na washindi wa medali za kimataifa, Ayatollah Khamenei aliwatambua vijana hao kama “nembo ya taifa na ishara ya uwezo wa kitaifa” akisema:

“Mumethibitisha kuwa vijana wa Iran wanaweza kusimama juu ya vilele vya dunia na kuvutia macho ya ulimwengu kuelekea nuru ya Iran.”

Kuhusu matamshi ya rais wa Marekani:

Ayatollah Khamenei alikosoa matamshi ya hivi karibuni ya rais wa Marekani kuhusu Iran na eneo la Asia ya Magharibi, akisema:

“Rais wa Marekani alisafiri hadi Palestina iliyovamiwa na kutoa maneno matupu yaliyofurika uongo na upuuzi, kwa lengo la kuwapa moyo Wazayuni waliokata tamaa.”

Amesema badala ya kuingilia masuala ya mataifa mengine, rais huyo anapaswa kwanza kutuliza mamia ya maelfu ya Wamarekani wanaoandamana dhidi yake katika majimbo mbalimbali.

Kuhusu nguvu za Iran na makombora yake:

Ayatollah Khamenei amesema:

“Wazayuni hawakutarajia kwamba makombora ya Iran yangepenya hadi kwenye maeneo yao nyeti na kuyaangamiza kabisa. Makombora haya hayakunuliwa wala kukodishwa - ni kazi ya vijana wa Iran wenye vipaji, waliotengeneza kila kitu kwa mikono yao.”

Ameongeza kuwa majeshi ya Iran bado yana uwezo na akiba ya kijeshi, na “kama ikihitajika, yataitumia tena nguvu hiyo kwa wakati unaofaa.”

Kuhusu Marekani na vita vya Gaza:

Kiongozi wa Mapinduzi amesema wazi kuwa Marekani ni mshirika mkuu wa jinai za utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza, akifichua kwamba silaha zilizotumika dhidi ya raia wasio na ulinzi zilikuwa za Marekani.

Ameuliza kwa ukali:

“Zaidi ya watoto 20,000 wameuawa Gaza — je, hao ni magaidi? Magaidi ni Marekani, ambayo ilianzisha kundi la ISIS na kulileta katika eneo hili kwa maslahi yake.”

Kuhusu madai ya Marekani juu ya nyuklia:

Ayatollah Khamenei alisema:

“Rais wa Marekani anadai kwa majivuno kwamba amebomoa miundombinu ya nyuklia ya Iran. Hata kama anafikiri hivyo, nani aliyempa mamlaka kuamua nini Iran inapaswa kuwa nacho? Suala la nyuklia la Iran halimhusu kabisa Marekani. Hizi ni siasa za kibabe na za kiimla.”

Kuhusu madai ya Marekani ya “kuunga mkono watu wa Iran”:

Ameita kauli hizo “uongo mkubwa”, akisema:

“Vikwazo vyao vinalenga moja kwa moja wananchi wa Iran. Wao ni maadui wa taifa la Iran, si marafiki.”

Kuhusu vita na vurugu katika Asia ya Magharibi:

Ayatollah Khamenei alisema:

“Ni Marekani inayochochea vita na vurugu katika eneo hili. Vituo vyake vya kijeshi vimezagaa kote Asia ya Magharibi - je, vinafanya nini hapa? Eneo hili ni mali ya watu wake, na kifo na vita vinavyoendelea ni matokeo ya uwepo wa Marekani.”

Hitimisho:

Kiongozi wa Mapinduzi alisisitiza kuwa matamshi ya rais wa Marekani ni ya uongo, ya kiburi, na ya kiimla, na akaongeza:

“Ingawa siasa za mabavu zinaweza kuathiri baadhi ya mataifa dhaifu, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, hazitawahi kuwa na athari yoyote kwa taifa lenye imani na uimara wa Iran.”

Katika hafla hiyo, timu ya vijana wa michezo ya jadi ya Iran (Pahlevani) ilifanya maonesho maalum ambayo yalipokelewa kwa pongezi kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha