Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (AS) -ABNA- Mkutano huo ulifanyika kati ya Qasim al-A’araji na ujumbe wake pamoja na Meja Jenerali Mohammad Pakpour, Kamanda Mkuu wa IRGC.
Qasim al-A’araji aliwasilisha salamu na saluti kutoka kwa Rais na Waziri Mkuu wa Iraq kwa Meja Jenerali Pakpour, akisisitiza dhamira ya Iraq katika kutekeleza makubaliano ya kiusalama na Iran. Alisema wazi kuwa “usalama wa Iran ni usalama wa Iraq,” na kukataa kwa uthabiti matumizi ya ardhi ya Iraq kwa shambulio lolote dhidi ya Iran. Pia alitangaza kuundwa kwa kamati ya pamoja ya kusimamia utekelezaji wa mkataba wa kiusalama kati ya nchi hizo mbili na kuzuia harakati zozote zisizo halali.
Aidha, al-A’araji alizungumzia makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, akionesha kutokuwa na imani na utawala wa Kizayuni na akionya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuvunjwa kwa makubaliano hayo. Alisisitiza kuwa umoja wa nchi za eneo hilo ndiyo ufunguo wa amani na utulivu. Aliongeza kuwa katika vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, adui alitarajia wananchi wa Iran waasi dhidi ya serikali yao, lakini wananchi walionesha mshikamano wa kitaifa na uaminifu wao kwa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Meja Jenerali Pakpour aliukaribisha ujumbe wa Iraq na kusema kuwa ziara hiyo ni muhimu sana katika kipindi hiki kwa Iraq. Alionya kuwa maadui wa eneo hili wanatafuta kudhoofisha umoja wa ndani wa mataifa. Akizungumzia vita vya siku 12, alisema kuwa utawala wa Kizayuni ulilenga kuua makamanda na kusababisha vurugu ili kuvuruga mshikamano wa kitaifa wa Iran, lakini njama hizo zilifeli kutokana na hekima ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi na umakini wa wananchi.
Kamanda huyo Mkuu wa IRGC alisema: “Adui alidhani nguvu zetu za makombora zingepungua katika siku za mwanzo, lakini tulionyesha nguvu na ukali mkubwa, na tuliharibu kwa usahihi malengo yote yaliyolengwa.” Aliongeza kuwa Iran ipo tayari kikamilifu kujibu kwa ukali uvamizi wowote wa baadaye, akisema: “Tukivamiwa, tutawasha moto wa Jahannam dhidi ya adui.”
Meja Jenerali Pakpour alishukuru Iraq kwa juhudi zake katika kudhibiti makundi ya waasi wakati wa vita vya siku 12, na akasisitiza umuhimu wa kutekeleza kwa ukamilifu makubaliano ya kiusalama na kuanzisha kamati ya ufuatiliaji wa mipaka. Alisema makundi hayo ni tishio kwa usalama wa nchi zote mbili na yanapaswa kudhibitiwa kwa ushirikiano wa karibu.
Kwa upande wake, al-A’araji alisisitiza tena kuwa Iraq imejitolea kuzuia ardhi yake kutumiwa kwa shambulio lolote dhidi ya Iran, akisema: “Katika vita vya siku 12 hatukuruhusu kundi lolote la waasi kufanya harakati, na tutaendelea kuzuia hilo kwa uthabiti.”
Mwisho wa mazungumzo hayo, pande zote mbili zilisisitiza kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na utekelezaji wa makubaliano ya pamoja, huku viongozi wa Iraq wakithibitisha uaminifu wao wa kisiasa na kimaadili kwa makubaliano na Iran.
Your Comment