Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Maafisa wa Marekani wamefikia hitimisho kwamba kuangamiza kijeshi Hamas na Hezbollah katika mazingira ya sasa hakuwezekani. Kwa sababu hiyo, mkazo wa sera za Washington umehama kutoka kwenye dhana ya “kukusanya silaha” kwenda kwenye mkakati wa “kuzuia matumizi ya silaha.”
Gazeti la Lebanon Al-Akhbar katika ripoti yake kuhusu safari ya Tom Barrack kwenda katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, lilibainisha kuwa safari hiyo - licha ya kelele za vyombo vya habari - haikuwa na ujumbe wa vitisho au mpango wa kulazimisha, bali ilikuwa ya mashauriano na tathmini. Kinyume na madai ya kuwepo kwa hati ya mwisho ya aina ya “kubali au kataa”, lengo la safari hiyo lilikuwa kupima misimamo ya utawala wa Israel, kubaini mistari yake myekundu, na kutathmini uwezo wa mazungumzo na njia za shinikizo. Safari hiyo pia imeelezwa kuwa ni maandalizi ya mkutano ujao kati ya Donald Trump na Benjamin Netanyahu.
Hata hivyo, safari hiyo imebeba ujumbe muhimu wa kimkakati. Serikali ya Trump haiangalii tena kwa mtazamo wa mafaili yaliyotenganishwa kuhusu Gaza, Lebanon na Syria, bali inayaona maeneo hayo kama sehemu za mfumo mmoja wa kiusalama katika muktadha wa mtazamo wa kikanda. Lengo la Marekani katika mkabala huu si tu kudhibiti mgogoro wa Gaza, bali ni kupanga upya mlinganyo wa usalama wa Asia Magharibi, kudhoofisha wapinzani wa Washington, na kuimarisha aina za maridhiano ya kudumu yanayohudumia maslahi yake.
Katika muktadha huu, Washington inafuata mkabala mpya unaoitwa “kufafanua upya suala la kuvua silaha.” Maafisa wa Marekani wamekubali kwamba kuangamiza kijeshi Hamas na Hezbollah kwa sasa si jambo linalowezekana; hivyo, mkazo umehamia katika kuzuia matumizi ya silaha badala ya kuzikusanya. Mabadiliko haya yanaashiria kukubaliwa kwa mipaka ya uhalisia wa uwanja wa mapambano, na kuelekea kwenye mifumo ya kuzuia na uangalizi badala ya suluhu za nguvu kali.
Njia hii, hasa katika suala la Gaza, inaweza kusababisha tofauti kati ya Marekani na Israel katika hatua ya pili ya usitishaji mapigano. Huko, Tel Aviv inafunga uondoaji wake kutoka baadhi ya maeneo ya Gaza na kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa na sharti la kuvuliwa silaha kwa Hamas, ilhali Washington kivitendo inatenganisha masuala hayo mawili. Tofauti hii inahitaji maamuzi ya ngazi ya juu ya uongozi wa nchi hizo mbili, na iko nje ya uwezo wa kutatuliwa na mjumbe mmoja.
Katika faili la Syria, ujumbe wa Marekani ni wazi: Syria ni sehemu isiyotenganishwa ya mlinganyo wa kikanda, na uthabiti wa serikali mpya chini ya uongozi wa Ahmad al-Sharaa ni jambo la msingi kwa maridhiano yoyote yajayo. Mtazamo huu unakinzana na msimamo wa Israel, ambayo inaiona serikali mpya ya Syria kuwa haina uwezo au haina nia ya kudhibiti vitisho vya mipakani, na kwa misingi hiyo inaendelea kuhalalisha operesheni za kijeshi kusini mwa Syria. Tofauti hii imekuwa moja ya changamoto kuu katika uhusiano kati ya Washington na Tel Aviv.

Your Comment