Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Hujjatul-Islam wal-Muslimin Syed Sajid Ali Naqvi, Mwenyekiti wa Shia Ulema Council Pakistan, ametangaza kuwa kupigwa marufuku kwa harakati ya Tehrik-e-Jafaria kumetekelezwa chini ya sera isiyo ya haki iitwayo “sera ya mizani (balance policy)” na kwamba hatua hiyo haina msingi wowote wa kisheria.
Amesisitiza kuwa harakati hiyo haina uhusiano wowote na ugaidi, misimamo mikali ya kimadhehebu au itikadi kali, na akaongeza kuwa kwa miaka mingi Mashia ndio wamekuwa wahanga wakuu wa mashambulizi ya kigaidi nchini Pakistan.
Naqvi alisema: jina la taasisi hiyo limewekwa kwa dhuluma katika orodha ya makundi yaliyopigwa marufuku, na hatua hiyo imewanyima maelfu ya watu haki zao za msingi na za uraia.
Akirejea historia ndefu ya Tehrik-e-Jafaria katika kuendeleza umoja wa Umma wa Kiislamu, alisema kuwa harakati hiyo ilikuwa miongoni mwa waanzilishi wa umoja baina ya Waislamu nchini Pakistan, na ilichukua nafasi muhimu katika Baraza la Mshikamano wa Kitaifa pamoja na Muungano wa Mabaraza ya Utekelezaji (Muttahida Majlis-e-Amal). Hata katika mazingira magumu ya kiusalama, si tu kwamba walisaini hati za umoja bali pia walizitekeleza kwa vitendo.
Naqvi aliongeza kuwa licha ya juhudi hizo zote, sera ya “mizani” imewaweka pamoja na makundi ya kitakfiri na yenye silaha, jambo alilolielezea kuwa ni dharau ya wazi kwa jamii ya Mashia.
Mwisho, alitaka uchunguzi wa haraka na wa uwazi kuhusu tukio la Tarlai, Islamabad (Msikiti na Imambargha ya Khadija al-Kubra), na akatangaza kuwa watachukua hatua za kisheria kupitia Mahakama Kuu ya Pakistan kupinga marufuku hiyo isiyo ya haki, ili kukomesha sera hiyo ya dhuluma na kurejesha imani ya umma pamoja na utawala wa sheria.
Inafaa kutajwa kuwa serikali ya Pakistan, ili kuepuka tuhuma za upendeleo wa kimadhehebu, inapoweka makundi ya misimamo mikali ya Kiwahabi kama vile Sipah-e-Sahaba Pakistan (ya zamani), Lashkar-e-Jhangvi na matawi ya kitakfiri katika orodha ya mashirika yaliyopigwa marufuku (proscribed), huongeza pia kwa wakati huo au kwa mtindo unaofanana majina ya makundi ya Kishia kama Tehrik-e-Jafaria Pakistan (TJP). Mtazamo huu unajulikana kama “sera ya mizani.” Jamii ya Mashia nchini Pakistan inaona sera hii kuwa ya dhuluma na isiyo ya haki kabisa, ikisisitiza kuwa taasisi za Kishia hazina historia ya vitendo vya kigaidi, bali kwa miaka mingi zimekuwa wahanga wakuu wa ugaidi na daima zimehimiza umoja wa Umma wa Kiislamu na mshikamano baina ya Waislamu.
Your Comment