29 Mei 2026 - 19:05
Iran Yapendekeza Mfumo Mpya wa Usalama wa Kikanda katika Mkutano wa BRICS Moscow

Naibu Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Bagheri, amesema pendekezo la Iran la kuanzisha mfumo mpya wa usalama katika eneo limepokelewa vyema katika mkutano wa kimataifa wa viongozi wa usalama wa BRICS uliofanyika Moscow, huku akisisitiza umuhimu wa kuondoa ushawishi wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Naibu Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia siasa za nje na usalama wa kimataifa, Ali Bagheri, amesema kuwa mkutano maalumu wa viongozi waandamizi wa usalama wa nchi za BRICS uliofanyika mjini Moscow ulikuwa wenye mafanikio makubwa na wenye kujadili kwa kina masuala muhimu ya kimataifa na kikanda.
 
Bagheri alieleza kuwa katika mikutano yake ya pembeni na viongozi mbalimbali wa usalama kutoka Asia, Afrika, Ulaya na Amerika ya Kusini, Iran iliwasilisha wazo la kuanzishwa kwa mfumo mpya wa usalama wa kikanda utakaotegemea ushirikiano wa mataifa ya eneo badala ya kuingiliwa na Marekani pamoja na ushawishi wa utawala wa Kizayuni.
 
Amesema mataifa mengi yaliyoshiriki mkutano huo yalilipokea vyema pendekezo hilo, hasa baada ya matukio ya hivi karibuni ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Iran na washirika wake.
 
Bagheri alisisitiza kuwa mfumo wa sasa wa usalama katika eneo umeshindwa kuleta amani na uthabiti, akidai kuwa uwepo wa kambi za kijeshi za Marekani pamoja na sera za upanuzi wa utawala wa Kizayuni ni chanzo kikuu cha machafuko katika Mashariki ya Kati.
 
Aidha, alieleza kuwa mkutano wa Moscow umegeuka kuwa jukwaa muhimu la mataifa huru yanayopinga sera za upande mmoja za Marekani, huku nchi mbalimbali zikieleza nia ya kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiusalama kwa misingi ya kuheshimiana na kulinda maslahi yao ya kitaifa.
 
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Bagheri alikosoa kile kilichoitwa “Makubaliano ya Ibrahim,” akisema kuwa hayajaleta amani ya kweli katika eneo, bali yameongeza hali ya kutokuwa na utulivu na migogoro ya kisiasa katika Mashariki ya Kati.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha