Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, timu ya taifa ya wanawake ya volleyball ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Wanawake ya CAVA 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa seti 3-1 dhidi ya Kazakhstan katika mchezo wa fainali uliofanyika Ijumaa mjini Kathmandu, Nepal.
Iran ilianza mchezo huo kwa nguvu kwa kushinda seti ya kwanza kwa alama 25-18, kabla ya Kazakhstan kusawazisha kwa kushinda seti ya pili 25-19. Hata hivyo, timu ya Iran ilirejea kwa kiwango cha juu na kushinda seti mbili zilizofuata kwa alama 25-15 na 25-21, na hivyo kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo.
Timu hiyo chini ya kocha mkuu kutoka Korea Kusini, Lee Do-hee, ilimaliza mashindano hayo bila kupoteza mchezo hata mmoja, ikipata ushindi dhidi ya Bangladesh, Sri Lanka, Nepal na Kazakhstan mara mbili, ikiwemo katika mchezo wa fainali.
Ushindi huo unaendelea kuidhihirisha Iran kama moja ya mataifa yanayokua kwa kasi katika mchezo wa volleyball ya wanawake katika ukanda wa Asia ya Kati. Mafanikio hayo pia yanakuja baada ya Iran kutwaa taji lake la kwanza la CAVA mwaka uliopita, ikiwa ni mafanikio makubwa katika historia ya volleyball ya wanawake nchini humo.
Baada ya kutwaa ubingwa huo, timu ya Iran inatarajiwa kuelekea nchini Ufilipino kwa ajili ya kambi maalumu ya maandalizi kabla ya kushiriki michuano ijayo ya Kombe la Volleyball la Wanawake la Asia.
Your Comment