Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania JMAT-TAIFA amesema kuwa hatua za Serikali kumchukulia mtu hatua za kisheria au kiusalama hazipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ni suala la udini. Katika ufafanuzi wake amebainisha kuwa, tawala nyingi duniani kwa kawaida hulinda maslahi yao na hupambana na yeyote wanayemwona kuwa anatishia au kuathiri maslahi hayo, na hawafanyi hivyo kwa kutizama huyu mtu ana dini gani.
Ameeleza kuwa historia ya Tanzania ina mifano ya watu wa dini mbalimbali waliokumbana na hatua za Serikali katika vipindi tofauti vya uongozi.
Katika muktadha huo, Sheikh Pro.Alhad Mussa Salum ametaja tukio la Askofu Ghwajima, kwamba ikiwa litachukuliwa kama hoja ya udini, basi inafaa pia yakumbukwe matukio yaliyowahusisha: Sheikh Ponda Issa Ponda (ambaye alipigwa risasi) na Masheikh wa Uamsho (ambao walifungwa miaka nane jela), yote hayo yalitokea wakati wa mtawala muislamu.
Sheikh Profesa Alhad akasisitiza kuwa matukio kama hayo hayapaswi kutumiwa kama ushahidi wa kuwepo kwa udini, bali yanapaswa kutazamwa kwa upana wake wa kisiasa na kisheria.
Aidha, Sheikh Profesa Alhad amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, akieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani kutokana na kuishi kwa upendo na kuheshimiana miongoni mwa wananchi wa dini tofauti. Ameongeza kuwa kuhubiri amani si udhaifu wala kutumwa na mtu yeyote, bali ni sehemu ya mafundisho ya dini ya Kiislamu ambayo yanahimiza wema, uadilifu na kuishi kwa amani na watu wote.
Your Comment