Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Ayatollah Ramezani ametoa taarifa kwa mnasaba wa kuuawa shahidi na kuzikwa kwa mwili mtakatifu wa kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akitoa salamu za rambirambi na masikitiko yake kwa Umma wa Kiislamu.
Andiko kamili la taarifa hiyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
(Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume yake, hao ndio wakweli na mashahidi mbele ya Mola wao. Wao watapata ujira wao na nuru yao. Na wale waliokufuru na wakazikanusha Aya zetu, hao ndio watu wa Jahannamu).
(An-Nisaa: 74)
Kuuawa shahidi kwa mja mwema wa Mwenyezi Mungu, mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Ali, Fatima na Husayn (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao), mwanachuoni na faqihi wa Kiungu, marjaa wa taqlidi wa wafuasi wa Ahlul-Bayt (as), mwanafikra mrekebishaji na mhuishaji, kiongozi wa Umma wa Kiislamu na kiongozi wa watu huru duniani, waliyyu faqih na mtawala mwadilifu, mpiganaji asiyekata tamaa, mwenye kuitambua vizuri mipango ya maadui na asiyechoka, mtetezi na msaidizi wa wanyonge, mataifa ya eneo hili, Muqawama dhidi ya ubeberu na haki na watu wa Palestina, mbeba bendera na alama ya kusubiri kudhihiri kwa Mahdi Anayesubiri (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), Imamu shahidi Ayatullah al-Uzma Sayyid Ali Husayni Khamenei, ni msiba wa kuhuzunisha na pengo lisiloweza kuzibwa katika Uislamu, kwa taifa la Iran, Umma wa Kiislamu na dunia.
Kuaga kwa kihistoria kwa watu wa Iran na Iraq na watu wote wa Umma wa Kiislamu, kuanzia Musalla Kuu ya Tehran, ambayo ni miongoni mwa kumbukumbu zilizoachwa na Imamu na kiongozi huyo shahidi, hadi kwenye ardhi ya Aali Muhammad, Qum Tukufu na Haram Tukufu ya Fatima Ma’suma (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) na Msikiti Mtukufu wa Jamkaran, hadi chini ya kuba la makaburi matakatifu ya mababu zake Ali, Husayn na Abbas (amani iwe juu yao) huko Najaf Tukufu na Karbala Tukufu, na juu ya mabega ya watu wenye shauku na waaminifu wa Iraq, na hadi Mashhad Tukufu ambako yeye, kama askari aliye katika safu ya kamanda wake, Anisul-Nufus na Shamsush-Shumus, katika ardhi ya Tus, alizikwa; baada ya maisha ya jihadi ya kielimu, kisiasa na ya uwanjani, juhudi za kuamsha Ulimwengu wa Kiislamu, uongozi na kutekeleza jukumu la kufundisha na kulea kwa namna ya kinabii, kuimarisha uelewa wa jamii ya Kiislamu na kuelekea katika ustaarabu mpya wa Kiislamu, kufafanua na kuongeza uelewa katika kufichua ujinga wa kisasa na kukabiliana nao, na utumwa wa zama mpya na ukoloni wa kizazi kipya, kupaza sauti na kusimama na kukabiliana na dhulma, udikteta na ubeberu, na muhimu zaidi ya yote, kuongoza na kuwa Imamu wa Umma; alikwenda kwa fahari kukutana na Mola wake, ili jina lake libaki milele katika historia kama mwanachuoni, marjaa, mtawala na kiongozi pekee aliyepata shahada baada ya babu yake, Amiri wa Waumini Ali (as).
Kuuawa shahidi kwa kiongozi mkuu wa Waislamu duniani kulikuwa mwanzo wa utume mpya wa watu wa Iran na Umma wa Kiislamu. Uwepo wa makumi ya mamilioni ya watu wapenda uhuru katika viwanja vyote vya Iran na kwa kipindi cha zaidi ya miezi minne, na katika tukio la kipekee la kumuaga Imamu shahidi na kuusindikiza mwili wake mtakatifu katika miji mitano ya nchi mbili, ambalo bila shaka, iwapo mazingira muhimu yangekuwepo, Umma wote wa Kiislamu ungependa kushiriki katika tukio hili la kihistoria lisilo na mfano; ni ishara ya utume mpya wa Umma, azma na utashi wa Waislamu na watu wote wapenda uhuru wa kupambana na ubeberu, Marekani yenye kutawala dunia na utawala haramu wa Kizayuni, kuendeleza njia iliyonyooka ya jihadi na kurejesha utukufu na ukuu wa Kiislamu, chini ya uongozi wa mrithi mwema wa kiongozi huyo, Mheshimiwa Ayatullah Sayyid Mojtaba Husayni Khamenei (Mwenyezi Mungu amuhifadhi), ambayo itaendelea hadi kufikiwa kwa ushindi, kuwekwa misingi ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, kusubiri kwa Mwokozi hadi kudhihiri kwake na kuanzishwa kwa dola tukufu ya uadilifu na usawa, ambayo ndiyo chanzo cha heshima ya Uislamu na watu wake.
Mimi, kwa niaba yangu, Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (as), na Mashia wote, Waislamu na wapenda uadilifu duniani, na kwa sauti moja na viongozi wote na wasomi wenye kujali maslahi ya Umma, nawapa shukrani zangu na pongezi kwa uwepo usio na mfano na ushiriki mkubwa na usio wa kawaida wa watu wote wa Iran na Umma wa Kiislamu, serikali na maafisa rasmi, viongozi wa kidini na viongozi wa kiroho wa dini na madhehebu mbalimbali, wanafikra na wasomi wa dunia, wapiganaji na wapenzi wote wa njia ya Imamu shahidi, ambao kwa ajili ya kutekeleza wajibu wao kwa kiongozi huyo aliyeandika historia, walijitwisha ugumu wa safari, mateso na changamoto za kushiriki katika tukio hili la kihistoria; na ninatumaini kwamba kwa moyo wao mpana na uvumilivu wao, watasamehe mapungufu yaliyotokea katika nchi ya Kiislamu ya Iran, katika mazingira magumu ya eneo na dunia.
Namuomba Mwenyezi Mungu Mwenye Uwezo wote atupe sisi sote tawfiki ya kuungana katika kutimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, kuendeleza njia ya Imamu huyo shahidi na kuliinua neno la Mwenyezi Mungu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh
Reza Ramezani
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (as)
Maoni yako