13 Desemba 2014 - 20:31
Daesh wadungua Helikopta ya jeshi la Iraq mjini Samarra

Maafisa nchini Iraq wamesema magaidi wa Daesh wamedungua helikopta ya jeshi na kuwauwa marubani wawili waliokuwemo.

Maafisa nchini Iraq wamesema magaidi wa Daesh wamedungua helikopta ya jeshi na kuwauwa marubani wawili waliokuwemo.

Shambulio hilo limezua wasiwasi mpya kuhusu uwezo wa kundi hilo kushambulia ndege wakati ambapo linakabiliwa na mashambulizi ya angani yanayoongozwa na Marekani.

Shambulizi la leo limetokea katika mji wa Washia wa Samarra, ulioko umbali wa kilomita 95 kaskazini mwa Baghdad. Afisa wa juu wa wizara ya ulinzi amesema katika maelezo yaliyothibitishwa na afisa wa jeshi, kuwa wapiganaji hao walitumia kombora la kufyatulia begani (RPG) kuidungua helikopta hiyo chapa ya EC635 katika kingo za mji huo.

Helikopta hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Airbus, imetengenezwa kwa ajili ya usafiri, uchunguzi na mapambano. Magaidi wa Daesh walidungua helikopta zisizopungua mbili karibu na mji wa Beiji mwezi Oktoba, na baadhi wanahofu huenda wapiganaji hao waliteka makombora yenye uwezo wa kushambulia ndege walipoteka vituo vya kijeshi nchini Iraq na Syria na wengine wanadhani kwamba huenda silaha zilizoshushwa na jeshi la Marekani kwa bahati mbaya katika himaya za magaidi hao ndio zinatumika kushambulia ndege hizo.

Lebo