Rais wa Marekani Barack Obama amesikitishwa sana na shambulizi ambalo mtu aliyekuwa na silaha amewauwa polisi wawili mjini New York wakati wakishika doria ndani ya gari lao.
Mkasa huo umefuatia wiki kadhaa za maandamano ya hasira kuhusiana na matukio ya polisi kuwauwa watu weusi ambao hawakuwa na silaha. Kamishna wa polisi wa New York Bill Bratton, amesema Ismaaiyl Brinsley, mwenye umri wa miaka 28, aliwapiga risasi kichwani polisi hao bila kuwepo onyo lolote, wala uchokozi. Brinsley, ambaye ni Mmarekani wa asili ya Kiafrika alimpiga risasi na kumjeruhi mchumbake wa zamani kabla ya kuwauwa polisi hao mjini Brookyln. Mshukiwa huyo baadae alijiua mwenyewe kwa risasi baada ya kukimbilia kwenye kituo cha treni zinazopita chini ya ardhi. Polisi imesema alikuwa ameweka ujumbe kwenye mtandao wa internet kuwa alipanga kuwauwa "nguruwe" wawili kama hatua ya kulipiza kisasi kifo cha Eric Garner, Mmarekani mweusi aliyeuawa kwa kukabwa koo na polisi.
Mauaji haya yanatokea baada ya serikali ya Marekani kufumbia macho malalamiko ya raia wake wenye asili ya kiafrika, ambao wameuawa kinyume na sheria na badala yake wauaji kuachwa huru na kuonekana kuwa hawajafanya makosa.