Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kwa nini kuwahudumia watu hakuchukua nafasi ya ibada?. Ikiwa mtu ana hamu ya kujiendeleza mwenyewe na pia kuendeleza malezi ya watoto wake kwa njia ya Kiislamu, au anataka kulea watu wa namna hiyo, ni muhimu sana kutilia maanani suala la maombi, dua, na ibada. Ibada si tu hisia halisi inayopandwa moyoni, bali ina athari kubwa katika nyanja nyingine za maisha ya mtu.
Hii ndiyo sababu viongozi wa dini hukumbusha daima: Hata kama una kazi nyingi kiasi gani, hakikisha unajipatia angalau saa moja kwa siku kwa ajili yako mwenyewe.
Labda unaweza kusema: “Siku zangu zote ni za kuwahudumia watu, sina hata saa moja kwa ajili yangu.”
Hapana! Hata kama mtu atajitolea muda wake wote kuhudumia viumbe wa Mwenyezi Mungu, bado hawezi kuepuka kuhitajia (au kutenga) saa moja kwa ajili yake mwenyewe. Saa hiyo, ingawa ni ya mtu binafsi, ni muhimu sana na haiwezi kuchukuliwa na shughuli nyingine—hata kama zile ni muhimu na zinahitajika. Saa moja tu hiyo —au zaidi— Mwanaadamu anapaswa kujiwekea wakati wa kuangalia ndani ya nafsi yake, kuondoa mawazo ya dunia, na kurudi kwa Mungu wake.
Katika wakati huo, awe peke yake na Mungu wake, akifanya maombi, manong’ono na Mola wake, na toba. Toba ni kujihesabu mwenyewe, kuangalia yaliyotendeka ndani ya saa 24 zilizopita: Ni kwanini nimefanya jambo fulani vizuri, na kumshukuru Mungu; na ni kwanini jambo fulani si vizuri kulifanya, hivyo utaamua kutolifanya au kama umelifanya basi utaamua kutoendelea kulifanya na kuomba msamaha.
Qur’an pia inatilia umuhimu mkubwa kwa suala la toba. Kuna msemo kuhusu Masahaba wa Mtume (s.a.w.w): - رُهْبانُ اللَّیلِ وَ اسْدُ النَّهارِ - “Wahamiaji wa usiku na simba wa mchana.”
Qur’ani inasema:
الصّابِرینَ وَ الصّادِقینَ وَ الْقانِتینَ وَ الْمُنْفِقینَ وَ الْمُسْتَغْفِرینَ بِالْاسْحارِ
"Wavumilivu (Wenye Subira), waaminifu (wasema kweli), watiifu, wasambazaji (misaada na sadaka), na wanaoomba msamaha alfajiri." (Aali Imran: Aya ya 17).
Angalia jinsi Qur’an inavyobainisha kila upande wa maisha ya Mwanadamu!
Chanzo:
Shahidi Mutahhari, Taelim na Tarbiyya katika Uislamu, ukurasa wa 228.
Your Comment