Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika makala rasmi kutoka katika Ofisi ya Ayatollah Makarim Shiraz, imetolewa hoja ya kupinga vikali dai la Qadhi Abubakr ibn al-Arabi al-Andalusi, ambaye alidai kuwa kuuawa kwa Imam Hussein (a.s) kulifanywa kwa mujibu wa hadithi ya Mtume (s.a.w.w) inayosema "mpasue umoja wa Umma apigwe kwa upanga", akidai kuwa Imam Hussein alivunja umoja wa Waislamu.
Hoja za Kimsingi za Kupinga Dai Hilo:
1. Yazid ndiye aliyesababisha mzozo wa mauaji hayo makubwa:
Historia inaonyesha wazi kuwa Yazid ndiye aliyeanzisha mzozo kwa kumtaka Imam Hussein (a.s) atoe kiapo cha utii (Baia) kwa nguvu, na alipokataa, alipewa vitisho vya kuuawa.
Hii ndiyo sababu iliyomfanya Imam Hussein (as) alazimike kuondoka Madina na kwenda al_Kufa.
2. Imam Hussein (a.s) ni msafi (mtoharifu) na hana makosa:
Kwa mujibu wa Aya ya "Tathira" (Qur’an, Ahzab: 33), Ahlul-Bayt (a.s), akiwemo Imam Hussein(as), wamesafishwa (wametakaswa) na Mwenyezi Mungu dhidi ya dhambi. Hivyo, haiwezekani Imam kuwa chanzo cha fitina au kuvunja umoja.
3. Lengo la Imam lilikuwa ni kutekeleza wajibu wa kidini:
Imam Hussein (a.s) aliondoka Madina kwa nia ya Amr bil Ma’ruf na Nahy anil Munkar (kuamrisha mema na kukataza maovu). Katika wasia wake kwa ndugu yake Muhammad bin al-Hanafiyya, alieleza bayana kuwa hakufanya hivyo kwa tamaa ya madaraka, bali kurekebisha hali ya Umma.
4. Utawala wa Yazid haukuwa halali:
Kwa mujibu wa makubaliano ya amani baina ya Imam Hassan (a.s) na Mu’awiyah, Yazid hakuwa na haki ya kurithi utawala. Aidha, alikuwa mlevi, mzinifu, na mwenye dhambi wazi, asiye na sifa za kuwa kiongozi wa Kiislamu.
5. Qadhi ibn al-Arabi alipuuzia Hadithi nyingine nyingi:
Alizingatia hadithi moja tu kuhusu “kuvunjika kwa umoja” na kupuuza hadithi nyingi za Mtume (s.a.w.w) kuhusu wajibu wa kukemea dhulma, kuamrisha mema, na kupinga viongozi waovu. Mfano:
“Yeyote atakayemuona kiongozi dhalimu anavunja sheria za Mwenyezi Mungu… halafu asimkeme kwa kauli au matendo, basi Allah atamhesabu miongoni mwao.”
6. Mtume (saww) mwenyewe alitoa wito wa kumuunga mkono Hussein (as):
Kuna hadithi kutoka kwa Mtume isemayo:
“Hakika mwanangu Hussein atauawa katika ardhi ya Iraq. Atakayemuona, basi amsaidie.”
Hitimisho:
Dai la Qadhi Abubakr bin al-Arabi kuwa kuuawa kwa Imam Hussein (a.s) ni halali ni batili na linalenga kutetea jinai ya Yazid. Kusimama kwa Imam Hussein (a.s) dhidi ya dhulma ilikuwa ni njia ya kuhuisha dini ya Kiislamu na siyo kuvunja umoja wa Waislamu. Kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa msafi ni uasi dhidi ya dini na uadilifu.
Kwa hiyo, Imam Hussein (a.s) alisimama kwa ajili ya haki, uadilifu na uhai wa Uislamu wa kweli — na alikumbatia shahada kwa ajili ya kuilinda dini ya babu yake Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Your Comment