17 Agosti 2025 - 22:27
Shukrani za Balozi wa Iran kwa Marjaa, Serikali na Wananchi wa Iraq kwa Kufanikisha Maadhimisho ya Arubaini

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Iraq, Bw. Muhammad Kazim Al-Sadiq, ametuma tamko maalum la shukrani kwa Marjaa wa kidini, serikali, wananchi, hasa makabila, vijana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Iraq kwa kufanikisha maadhimisho ya Arubaini ya Imam Hussein (a.s).

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Balozi Al-Sadiq alisifu ukarimu na ugeni wa kipekee wa wananchi wa Iraq na kueleza kuwa maadhimisho haya ni alama ya umoja na msimamo wa pamoja dhidi ya maadui wa eneo. Aidha, aliwashukuru pia mahujaji wa Kiirani kwa ushiriki wao wenye nidhamu na heshima.

Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Iraq, Balozi Al-Sadiq katika tamko lake alisema:

“Kwa Jina la Mola wake Hussein (a.s) na kwa kumbukumbu ya wito wa mashujaa waliolijibu sauti ya ‘Hal min nasirin yansuruni’ – je, kuna wa kunisaidia? – tunathibitisha upya ahadi tuliyoikubali kwa imani na tutaendelea kusimama imara juu yake. Ni ahadi tuliyoifunga kwa nafsi zetu na kwa moyo tunasema: Tupo thabiti juu ya mkataba huo.”

Balozi huyo aliongeza:
Katika safari hii ya kuelekea Karbala, maana halisi ya mapenzi na ikhlasi inajitokeza. Miongoni mwa mandhari yote ya kupendeza ya Arubaini, sura ya nyoyo safi za wana wa Iraq ndiyo iliyo bora zaidi. Enyi wenye mahema na mahekalu ya Arubaini, ninyi ndio wenyeji waaminifu wa njia hii ya nuru, njia ya kudhihiri kwa Mahdi (a.f). Hamkufungua tu milango ya nyumba zenu, bali pia nyoyo zenu kwa wageni. Kwa kipande cha mkate, kikombe cha maji na mkeka wa udongo, lakini kwa mikono iliyojaa mapenzi na macho yenye nuru ya mbinguni, mmefundisha ulimwengu maana ya ukarimu, heshima na upaji.”

Al-Sadiq aliendelea kusema:
“Mmetufundisha kwamba huduma kwa Hussein (a.s) haina mipaka. Enyi wana wa ukarimu, tumekujifunzeni mapenzi na udugu. Nyoyo zenu zimekuwa za Husayni na bila ya matarajio yoyote wala taklifu, mmewapokea mahujaji wa Hussein (a.s). Kutoka kwenye undani wa nyoyo zetu, kupitia machozi na elimu ya maarifa, tunasema: Enyi watu wa Iraq, tunawashukuruni. Kuanzia Marjaa wakuu, serikali na wananchi, hadi makabila jasiri, vijana wenye hamasa, akina dada wa Kishujaa wa Zaynabi na maafisa wote wa ulinzi na usalama – macho hayo yasiyolala, yaliyokesha usiku kucha kuhakikisha usalama wa mahujaji na kuyafukuza mawingu ya giza, ujinga na chuki.”

“Enyi wananchi watukufu wa Iraq, tunabusu udongo wa nyayo zenu kwani mmelipamba njia ya Hussein (a.s) kwa maua. Mchanganyiko huu wa ajabu wa meza za ukarimu wa Hussein (a.s) uliojaa hisani, roho na msimamo, unarudia neno ‘Haihat minna dh-dhilla’ – kamwe hatutakubali fedheha. Neno hili leo limeyumbisha nguzo za maadui wa umma wetu katika eneo na limefichua kushindwa kwao katika kueneza fitna kati ya mataifa. Na InshaAllah, kwa kuiga harakati ya Hussein (a.s), bendera za dhulma na uvamizi zitang’olewa kutoka katika eneo hili.”

Katika hitimisho la ujumbe wake, Balozi wa Iran alisema:
“Lazima pia nitoe shukrani kwa taifa letu tukufu la Iran kwa kushiriki kwa hekima, maarifa, heshima na utulivu katika mapinduzi haya makubwa ya Arubaini ya Sayyid al-Shuhadaa (a.s). Mmeheshimu sheria na desturi zote za nchi rafiki na ndugu, Iraq, na nawambia: nyinyi ni chachu ya fahari na utukufu.”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha