Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (as) -ABNA- Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linafanya kura ya maamuzi kuhusu kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, kutokana na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, baada ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kuanzisha rasmi mfumo wa kichocheo (snapback mechanism).
Uenyekiti wa sasa wa Baraza umetangaza kwamba kikao cha kujadili suala la vikwazo kimepangwa kuanza leo Ijumaa saa 14:00 GMT.
Kwa mujibu wa Azimio la 2231, ambalo ndilo msingi wa kisheria wa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, rasimu ya azimio itawekwa mbele ya wajumbe ili kupigiwa kura. Rasimu hiyo inalenga kuendeleza hali ya sasa ya kusitishwa kwa vikwazo.
Ili azimio hilo lipitishwe, linahitaji angalau kura 9 za ndio kutoka kwa jumla ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama. Hata hivyo, vyanzo vya kidiplomasia vimeiambia shirika la habari la Ufaransa (AFP) kwamba uungwaji mkono wa kutosha haupo, jambo ambalo litapelekea kurejeshwa kwa vikwazo.
Kukwama kwa azimio hilo kutamaanisha kuwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vitarudi kabla ya mwisho wa wiki ijayo, isipokuwa kama mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa — ambapo Dkt. Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, atahudhuria — utaweza kufanikisha mazungumzo mapya na yenye mafanikio.
Taarifa rasmi iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama imetoa muda wa siku 30 kwa mchakato huo, ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki ijayo.
Katika mwisho wa mwezi Agosti, Troika ya Ulaya (yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) ilianzisha rasmi mfumo wa "snapback" au "machanizimu wa kichocheo", hatua inayowezesha kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya Iran, na nchi hizi zilianza tena vikwazo vyao binafsi dhidi ya Tehran.
Your Comment