Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Muhammad Shia’ al-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, amewaonya raia wa nchi hiyo dhidi ya kutoshiriki katika uchaguzi wa bunge wa Iraq uliopangwa kufanyika mwezi Novemba ujao. Alisisitiza kuwa kususia uchaguzi kutakuwa ni zawadi kwa mafisadi na wale wanaofanya kazi kinyume na maslahi ya Taifa.
Katika mkutano wake na viongozi wa koo, wazee wa kijadi, na wasomi wa vyuo vikuu wa eneo la Karrada, Baghdad, al-Sudani alisema:
“Leo hii, dunia inaiheshimu Iraq kutokana na mafanikio ambayo imepata katika nyanja mbalimbali.”
Alisisitiza pia juu ya umuhimu wa kushiriki kwa uelewa katika uchaguzi, akieleza kuwa:
“Kushiriki katika uchaguzi na kufanya chaguo sahihi ni hatua ya kwanza ya kuelekea usalama, uthabiti, maendeleo na kuepuka makosa ya zamani.”
Maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji
Waziri Mkuu aliongeza kuwa uwepo wa kampuni kubwa za kimataifa nchini Iraq ni dalili ya kuboreka kwa hali ya usalama na kiuchumi.
Alisema kuwa:
“Kufikia kiwango cha uwekezaji cha dola bilioni 100 ni ushahidi kuwa Iraq ni nchi salama, thabiti, na mazingira yake yanavutia kwa wawekezaji.”
Al-Sudani aliifananisha Iraq na “karakana kubwa” na kueleza kuwa katika mikoa yote ya nchi, miradi mbalimbali ya huduma inaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa mpango uliopangwa vizuri.
Historia fupi ya uchaguzi nchini Iraq:
Uchaguzi wa mwisho wa bunge ulifanyika tarehe 10 Oktoba 2021, kufuatia maandamano makubwa ya wananchi na kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Adel Abdul-Mahdi.
Baada ya kujiuzulu kwake, Mustafa al-Kadhimi aliteuliwa kuongoza serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi huo.
Bunge la sasa la Iraq lina wabunge 329, ambapo mabunge mengi yanatokana na vyama na vuguvugu vya Kishia.
Kwa mujibu wa utaratibu wa kisiasa wa Iraq:
1- Rais hutoka kwa Wakurdi.
2- Waziri Mkuu hutoka kwa Waislamu wa Madhehebu ya Shia.
3- Spika wa Bunge hupewa Waislamu wa Madhehebu ya Sunni.
Your Comment