Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la AhlulBayt (as) -ABNA- Gazeti la "Al-Akhbar" la Lebanon limenukuu vyanzo vya kijasusi mjini Sana'a vikiripoti kuwa Marekani na Israel wameanzisha tena vyumba vya operesheni vinavyosimamiwa na maafisa wa Imarati katika kisiwa cha Zuqar – kilichoko kwenye Bahari Nyekundu na ni sehemu ya visiwa vya Hanish – kwa ajili ya kuendesha oparesheni za kijasusi dhidi ya harakati ya Ansarullah.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Falme za Kiarabu (UAE) pia zimeongeza kituo cha onyo la mapema katika muundo huo, kwa ajili ya kufuatilia lolote linalohusu kurushwa kwa makombora au droni kutoka kwa wapiganaji wa Yemen dhidi ya Israel au meli zake kwenye Bahari Nyekundu. Kisiwa cha Zuqar sasa kimegeuzwa kuwa kituo cha juu cha upelelezi na ukusanyaji taarifa za kisasa.
Aidha, kikosi kinachoitwa “400” ambacho UAE ilikianzisha mwanzoni mwa mwaka 2021 kama kikosi cha kijasusi chini ya mwamvuli wa “kupambana na ugaidi”, ambacho kilikuwa kikitekeleza oparesheni kwa niaba ya Makao Makuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) katika pwani ya magharibi ya Yemen, hivi karibuni kimeanza tena kufanya kazi. Hatua hii imechukuliwa katika juhudi za Marekani za kudhoofisha uungwaji mkono wa Yemen kwa Ukanda wa Gaza.
Sambamba na harakati hizi, serikali ya Yemen imekuwa ikifuatilia kwa miezi kadhaa shughuli za kutiliwa shaka katika mikoa ya Shabwah, Hadhramaut na Al-Mahrah. Miongoni mwao ni kwamba UAE imeigeuza kambi ya "Marrah" huko Shabwah – ambayo hapo awali ilikuwa chini ya udhibiti wake – kuwa kituo cha kisasa cha kijasusi kilichounganishwa na Makao Makuu ya Jeshi la Marekani. Mwanaaktivisti wa Yemen, Ali Al-Nassi, katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii alifichua kuwa kituo hiki, kinachojulikana kama tovuti “C”, kinajumuisha vyumba vya operesheni na mawasiliano vilivyounganishwa na setilaiti, na wanajeshi wa UAE hawaruhusu hata washirika wao wa Yemen kuingia ndani.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen pia, siku mbili zilizopita, ilitoa onyo kuhusu njama za kulenga usalama wa ndani na mstari wa uungwaji mkono wa Yemen. Wizara hiyo ilitangaza kuwa mipango ya maadui inalenga kuzuia uungaji mkono wa wananchi wa Yemen kwa watu wa Palestina, lakini ikaongeza kuwa wako tayari kabisa kuvuruga njama hizo. Katika taarifa hiyo, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu zilituhumiwa kufadhili mipango hiyo kwa maslahi ya Marekani na Israel.
Kwa upande mwingine, vyanzo vya kijeshi vya Yemen viliiambia gazeti la "Al-Akhbar" kuwa juhudi za ulinzi za Yemen kwa ajili ya kulinda mstari wa msaada wa kijeshi kwa Gaza si ndogo ukilinganisha na oparesheni zenyewe. Vyanzo hivyo vilibainisha kuwa harakati ya Ansarullah inakabiliana na mfumo wa kimataifa unaolenga kuivuruga mstari wa Yemen. Pia walieleza kuwa kuna harakati kubwa zinazoongozwa na Makao Makuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) na Ubalozi wa Marekani nchini Yemen kwa kushirikiana na wapinzani wa Ansarullah, huku kipaumbele kikiwa ni ushirikiano wa kijasusi.
Hapo awali, CENTCOM ilikuwa imetangaza kupitia jukwaa la "X" (zamani Twitter) kuwa Admiral Brad Cooper, kamanda wa CENTCOM, alikutana na Meja Jenerali Sagheer bin Aziz, mkuu wa majeshi yanayohusiana na muungano wa Saudi–UAE. Kikao hicho, kilichofanyika kwa lengo la uratibu wa kijeshi na kiusalama pamoja na ushirikiano wa Marekani na serikali ya Aden, kilijadili masuala ya usalama na kijeshi kati ya pande hizo mbili.
Your Comment