Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Matamshi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu yametolewa leo asubuhi katika mji wa Qom, wakati wa kikao na waandaaji wa Kongamano la Kimataifa la Allamah Mirza Naeini (r.a).
Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei, katika mazungumzo hayo, alimuelezea Allamah Mirza Naeini kuwa ni miongoni mwa nguzo kuu za kielimu na kiroho wa Hawza kongwe ya Najaf, na akisema kuhusu sifa zake kwamba:
“Kwa upande wa kielimu, miongoni mwa sifa mashuhuri za marehemu Naeini ni uwezo wake wa kuunda mfumo wa kielimu katika fani ya Usul al-Fiqh, uliotegemea mpangilio wa fikra na elimu, pamoja na ubunifu wake mwingi na wenye nguvu.”
Kiongozi wa Mapinduzi pia alitaja malezi ya wanafunzi bora kuwa ni moja ya sifa nyingine muhimu za Allamah Naeini, na akaongeza:
“Sifa nyingine iliyomtambulisha kama mtu wa kipekee miongoni mwa wanazuoni wa kidini ni kuwa na mtazamo wa kisiasa wa kipekee, jambo lililodhihirika katika kitabu chake mashuhuri lakini kilichosahaulika ‘Tanbih al-Ummah’.”
Ayatullah Khamenei alibainisha kuwa, imani ya Allamah Naeini katika uundaji wa Serikali ya Kiislamu yenye msingi wa uongozi wa kisheria (Wilayah) dhidi ya udikteta, ilikuwa ni mhimili wa fikra zake za kisiasa.
Akaongeza kuwa: “Kwa mujibu wa fikra za kisiasa za marehemu Naeini, serikali na viongozi wake wote wanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa wananchi na wawajibike kwao. Hili linahitaji kuwepo kwa bunge la wawakilishi litakaloundwa kupitia uchaguzi, kwa ajili ya usimamizi na kutunga sheria. Hata hivyo, uhalali wa sheria za bunge hilo unategemea idhini ya wanazuoni na mafaqihi wakubwa wa dini.”
Kiongozi huyo alisema kwamba mfumo wa serikali uliopendekezwa na Allamah Naeini, yaani serikali ya Kiislamu yenye ushiriki wa wananchi, kwa lugha ya kisasa ni sawa na Jamhuri ya Kiislamu.
Akitaja sababu ya marehemu Naeini mwenyewe kukusanya tena kitabu chake “Tanbih al-Ummah”, alisema:
“Mapinduzi ya Kikatiba (Mashrutiya) ambayo Naeini na wanazuoni wa Najaf waliyaunga mkono, yalikuwa ni juhudi za kuanzisha serikali ya haki na kuondoa udikteta. Hayo yalikuwa tofauti kabisa na kile ambacho Waingereza waliita ‘Mapinduzi ya Kikatiba’ nchini Iran, ambayo yalipelekea migogoro na matukio machungu kama kunyongwa kwa Sheikh Fadlullah Nuri (r.a).”
Katika kikao hicho, Ayatullah A’rafi, Mkurugenzi wa Vyuo vya Kidini (Hawza) nchini Iran, alitoa ripoti kuhusu maandalizi na shughuli za Kongamano la Kimataifa la Kumkumbuka Allamah Naeini.
Your Comment