Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa kujiingiza kwa Sara Netanyahu, mke wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katika uteuzi wa Ronen Gofman kuwa Mkuu wa taasisi ya ujasusi ya Mossad kumezua dhoruba ya kisiasa na kiusalama ndani ya Israel.
Kwa mujibu wa gazeti la Israel Maariv, kufichuliwa kwa mkutano mrefu kati ya Ronen Gofman na Sara Netanyahu uliofanyika kabla ya tangazo rasmi la uteuzi wake na Benjamin Netanyahu, kumeibua maswali mazito ndani ya vyombo vya usalama vya Israel.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mkutano huo ulifanyika kabla ya Waziri Mkuu kutangaza rasmi uteuzi wa Gofman, jambo lililozusha mashaka kuhusu uwazi wa mchakato wa uteuzi katika taasisi nyeti za usalama. Tukio hili limefufua tena faili za zamani za madai ya ushawishi wa Sara Netanyahu katika uteuzi wa maafisa wa ngazi za juu za usalama.
Katika sehemu nyingine ya ripoti hiyo, gazeti hilo limerejea kisa cha Yossi Cohen, aliyekuwa Mkuu wa Mossad hapo awali, ambapo kwa mujibu wa ushuhuda wa mwaka 2013, alilazimika kutoa ahadi ya utii binafsi kwa Benjamin na Sara Netanyahu ili kuhakikisha uteuzi wake kuwa Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa.
Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Mossad kabla yake, Meir Dagan, aliwahi kusimulia kuwa Sara Netanyahu aliingia ghafla katika kikao cha siri kati yake na Waziri Mkuu, na Netanyahu akamwambia: “Yeye ni mshirika katika kila jambo.”
Ronen Gofman anakuwa Mkuu wa pili wa Mossad kuteuliwa kutoka nje ya mfumo wa ndani wa taasisi hiyo, na anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake mwezi Juni 2026 (sawa na miezi ya Dhul-Qa’dah na Dhul-Hijjah 1447 Hijria).
Ingawa muungano wa utawala umepongeza uteuzi huo, ndani ya taasisi ya Mossad mwenyewe kuna mshangao mkubwa pamoja na maswali mengi mazito kuhusu uhalali na mchakato wa uteuzi huo.
Your Comment