14 Desemba 2025 - 21:43
Mufti Mkuu wa Australia alilaani shambulio la silaha huko Sydney

Mufti Mkuu wa Australia na New Zealand amelilaani vikali shambulio la silaha lililotokea katika Ufukwe wa Bondi, Sydney, na kulitaja kuwa ni kitendo cha kigaidi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Mufti Mkuu wa Australia na New Zealand amelilaani kwa ukali shambulio la silaha lililotokea katika Ufukwe wa Bondi, mjini Sydney, na kulielezea kuwa ni kitendo cha kigaidi na cha kipumbavu.

Dkt. Ibrahim Abu Mohammad, Mufti Mkuu wa Australia na New Zealand, katika mahojiano na mtandao wa Al Jazeera, akirejelea tukio la ufyatuaji risasi lililotokea leo Jumapili katika Ufukwe wa Bondi, alisema: “Tunalilaani vikali shambulio hili na tunatoa pole na rambirambi zetu kwa familia za waathirika.”

Aliongeza matumaini yake kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa ukali kamili dhidi ya wahusika wa tukio hili na kwamba haki itatekelezwa katika kesi hii.

Abu Mohammad, akizungumza kuhusu mawasiliano yake na maafisa wa Australia, alisema kuwa polisi wa nchi hiyo walimpa kwa simu maelezo ya shambulio hilo, na baada ya hapo alitoa tamko la kulaani kitendo hicho.

Alisisitiza: “Tunalaani kila tendo ovu linalomdhuru binadamu yeyote, bila kujali dini, utaifa au utambulisho wake.”

Mufti Mkuu wa Australia na New Zealand pia alitangaza kuwa amewasiliana na jamii ya Wayahudi wa Australia na kusema: “Tumetangaza mshikamano wetu kamili nao na kuwaambia kuwa tunashiriki pamoja nao katika huzuni na maumivu yao. Hakuna binadamu anayepaswa kulengwa kwa sababu ya dini, utaifa au mfungamano wake wa kijamii.”

Alilitaja shambulio hilo kuwa ni uvamizi dhidi ya raia wote huru wa Australia, na akaongeza: “Sisi daima tunatofautisha kati ya uraia wa Australia na matukio ya Mashariki ya Kati, na hatutaki yale yanayotokea Mashariki ya Kati yaingie ndani ya jamii ya Australia.”

Abu Mohammad pia alisema kuwa jamii ya Waislamu wa Australia baada ya tukio hili inahisi wasiwasi, na akasisitiza kwamba hawajawahi kutamani shambulio kama hilo litokee wala mtu yeyote kutoka jamii ya Waislamu ahusishwe nalo.

Aliongeza: “Uwendawazimu huu umewadhuru watu wasio na hatia waliokuwa tu katika sherehe na furaha.”

Kwa mara nyingine alisisitiza: “Kwa mtazamo wetu, haijalishi kama mwathirika ni Mwislamu au Myahudi; uhalifu ni uhalifu.”

Wakati huo huo, maafisa wa Australia walitangaza kuwa katika tukio hili la ufyatuaji risasi, lililotokea sambamba na sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah (Sikukuu ya Nuru), watu 12 waliuawa na zaidi ya 10 kujeruhiwa, miongoni mwa majeruhi hao wakiwemo askari wawili wa polisi.

Polisi wa Australia walitangaza kuwa mmoja wa washambuliaji ameuawa, na mshukiwa wa pili amekamatwa akiwa katika hali mbaya. Vyombo vya habari vya ndani pia viliripoti kuwa utambulisho wa mmoja wa washambuliaji umetajwa kuwa ni “Navid Akram.”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha