Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Hizbullah ya Lebanon leo Alhamisi imetoa tamko kali ikilaani vikali kitendo cha kudharau Qur’ani Tukufu, na kukitaja kuwa ni uhalifu mchafu dhidi ya takatifu zaidi miongoni mwa matakatifu ya Waislamu.
Siku chache zilizopita, mgombea mmoja wa uchaguzi ujao wa Bunge la Marekani (Congress), kwa lengo la kuvutia makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali, alichoma moto Qur’an Tukufu hadharani. Wakati wa kitendo hicho, alidai kuwa endapo atashinda uchaguzi, ataumaliza kabisa uwepo wa Uislamu katika jimbo la Texas.
Mwanasiasa huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu, ambaye pia ana historia ya kumuunga mkono Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, alidai kuwa Waislamu wanajaribu kuteka na kutawala nchi za Kikristo.
Kitendo hiki cha kuchochea chuki kilikabiliwa na lawama kali kutoka kwa viongozi wa kisiasa, makundi ya kidini, pamoja na watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Hizbullah ya Lebanon katika tamko lake imesisitiza kuwa: “Utamaduni wa ubaguzi wa rangi na hotuba za chuki, ambazo zimekuwa zikichochewa na mikondo ya kisiasa na vyombo vya habari vya Magharibi kwa msukumo wa tawala mfululizo za Marekani na lobi za Kizayuni kwa miongo kadhaa, zimefanya juhudi za makusudi za kupotosha taswira ya Uislamu. Hatua hizi zinafanywa kwa ajili ya kutumikia miradi ya fitna, ukoloni na uharibifu, na ndizo sababu kuu zilizowapa ujasiri watu wenye misimamo mikali kufanya vitendo hivi vya aibu.”
Katika siku za hivi karibuni, maandamano makubwa pia yalifanyika mjini Sana’a, Yemen, yakilaani mfululizo wa matusi na uharibifu unaolenga Qur’ani Tukufu. Washiriki wa maandamano hayo, yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Sana’a, walilaani vikali vitendo hivyo na kusisitiza dhamira yao ya kuchukua msimamo madhubuti na wa uelewa dhidi ya vita vya Kizayuni.
Tamko la mwisho la maandamano hayo liliwataka mataifa yote na wasomi, hususan vyuo vikuu, kuonyesha hasira yao dhidi ya matusi hayo na kuimarisha uhusiano wao na Qur’ani Tukufu. Pia ilisisitiza kuwa ukimya na uzembe mbele ya uhalifu huu huudhalilisha utu na dini ya Umma wa Kiislamu.
Kwa upande wake, Sayyid Abdulmalik Badruddin Al-Houthi, kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, alilaani vikali kitendo cha mgombea huyo wa Marekani cha kuitukana Qur’ani Tukufu, akikitaja kuwa ni sehemu ya vita vilivyopangwa dhidi ya matakatifu ya Kiislamu. Alibainisha kuwa uhalifu huo wa kutisha ni sehemu ya vita endelevu vya Kiyahudi-Kizayuni dhidi ya Uislamu, na akataka kuchukuliwa misimamo thabiti dhidi ya vitendo hivyo.
Matukio haya yanaonesha kwa uwazi mvutano mkubwa uliopo ndani ya jamii ya Marekani pamoja na kuenea kwa chuki katika ngazi ya kimataifa, jambo linalohitaji umakini na hatua za haraka zaidi.
Aidha, Bunge la Yemen pia lililaani vikali kudharau Qur’ani Tukufu kulikofanywa na mgombea wa uchaguzi ujao wa Congress ya Marekani, pamoja na ukimya wa kimataifa mbele ya uchochezi huo wa wazi. Bunge hilo lilisisitiza kuwa nchi za Kiarabu na Kiislamu zinapaswa kuchukua msimamo wa vitendo, thabiti na wa pamoja dhidi ya mashambulizi ya kimfumo ya Kizayuni yanayolenga matakatifu ya Kiislamu.
Your Comment