29 Mei 2026 - 15:40
Iran: Mfumo wa Sasa wa Utawala wa Dunia Unakabiliwa na Mgogoro wa Imani na Uhalali

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema jamii ya kimataifa inashuhudia kuongezeka kwa migogoro, ukosefu wa usawa na kudhoofika kwa diplomasia, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa kweli wa kimataifa.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- , Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, amesema kuwa jamii ya kimataifa kwa sasa inakabiliwa si tu na migogoro mbalimbali ya kidunia, bali pia na ongezeko la mgogoro wa imani na uhalali wa mfumo wa sasa wa utawala wa kimataifa.

Akizungumza katika mkutano wa “Kundi la Marafiki wa Utawala wa Kimataifa” uliofanyika siku ya Alhamisi kwa saa za ndani, Iravani aliishukuru China kwa kuandaa mkutano huo pamoja na kuendelea kuunga mkono mfumo wa ushirikiano wa kimataifa na mataifa yanayoendelea.

Balozi huyo wa Iran alieleza kuwa dunia hivi sasa inashuhudia hali ya migongano mikubwa, ikiwemo mfumo wa upande mmoja badala ya ushirikiano wa kweli wa kimataifa, pamoja na kuongezeka kwa vikwazo, ushuru mkubwa na sera za kujilinda kiuchumi badala ya mazungumzo na diplomasia.

Aidha, alisema kuwa pengo la kifedha, utekelezaji wa sheria za kimataifa kwa upendeleo, pamoja na ushiriki usio sawa katika maamuzi ya kimataifa vinaendelea kuongeza kutokuaminiana na hali ya sintofahamu duniani.

Iravani aliongeza kuwa changamoto hizo zimechangia kuongezeka kwa umaskini, madeni makubwa, mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kivita, pengo la kidijitali na vita vya uchokozi, huku mataifa yanayoendelea yakiwa ndiyo yanayobeba athari kubwa zaidi.

Akizungumzia hali ya Iran, balozi huyo alisema kuwa uchokozi wa hivi karibuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unapaswa kutazamwa katika muktadha wa kudhoofishwa kwa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa na kupungua kwa heshima kwa diplomasia na sheria za kimataifa.

Alisisitiza kuwa wakati Iran ilikuwa ikishiriki katika mazungumzo na diplomasia, ilikumbwa na mashambulizi ya kijeshi na hatua za kichokozi.
Mwisho, Iravani alieleza kuwa utawala wa kweli wa kimataifa unapaswa kujengwa juu ya kuheshimu sheria za kimataifa, usawa wa mataifa, kutatua migogoro kwa njia za amani, pamoja na kuhakikisha maendeleo endelevu, haki ya tabianchi, usawa wa kidijitali na ustawi wa pamoja kwa mataifa yote duniani.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha