9 Juni 2026 - 21:39
Dua ya Kwanza ya Siku ya Mubahala: Njia ya Kumtambua Ahlul-Bayt (a.s.)

Miongoni mwa amali za Siku ya Mubahala kuna dua mbili zinazosomwa baada ya swala. Dua ya kwanza, ambayo haijulikani sana, inahusishwa na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuongozwa kwenye maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s.) na kubainisha nafasi yao ya kipekee katika Uislamu.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- , pamoja na amali zinazojulikana za Siku ya Mubahala kama vile kuoga (ghuslu) na kufunga, zimepokelewa pia dua mbili maalumu zinazopendekezwa kusomwa baada ya swala katika siku hiyo yenye umuhimu mkubwa katika historia ya Uislamu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya Kiislamu, dua ya pili ndiyo inayopatikana katika kitabu cha Mafatih al-Jinan, lakini dua ya kwanza ni ile ambayo marehemu Sheikh Abbas Qummi (Ra) aliitaja kwa jina lake tu la mwanzo, “Alhamdulillahi Rabbil-'Alamin”, bila kuleta matini yake kamili. Matini kamili ya dua hiyo imehifadhiwa katika kitabu Iqbal al-A'mal kilichoandikwa na Sayyid Ibn Tawus.

Dua hii adhimu husomwa kwa kusimama na kuelekeza uso mbinguni. Maudhui yake makuu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwondoa mwanadamu katika giza la ujinga na kumjaalia neema ya kuwatambua Ahlul-Bayt (a.s.) wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Wanazuoni wameeleza kuwa siri kubwa ya dua hii imo katika kuunganisha Aya tatu muhimu za Qur'ani Tukufu zinazohusiana na Wilaya na nafasi ya Ahlul-Bayt (a.s.), ambazo ni Aya ya Mawadda (mapenzi kwa Ahlul-Bayt), Aya ya Tat'hir (utakaso wa Ahlul-Bayt) na Aya ya Mubahala.

Kupitia Aya hizi, dua hiyo inasisitiza hadhi ya familia ya Mtume (s.a.w.w.) kama watu waliotakaswa na Mwenyezi Mungu na wafasiri wa kweli wa Qur'ani Tukufu.

Siku ya Mubahala huadhimishwa kila mwaka na Waislamu wengi duniani kama kumbukumbu ya tukio la kihistoria lililotokea kati ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na wajumbe wa Wakristo wa Najran, ambapo Ahlul-Bayt (a.s.) walishiriki katika tukio hilo muhimu lililotajwa ndani ya Qur'ani Tukufu.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha