Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA–, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mujtaba al-Husseini Khamenei, ametoa tamko maalumu kufuatia mazishi makubwa ya Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei (Quddisa Sirruhu), yaliyofanyika nchini Iran na Iraq kwa ushiriki wa mamilioni ya waombolezaji.
Mwanzoni mwa tamko lake, Ayatollah Sayyid Mujtaba al-Husseini Khamenei alitoa salamu kwa Imam Husayn (a.s.) na Ahlul-Bayt (a.s.), akieleza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitokana na mwamko wa Ashura na yamejengwa juu ya misingi ya harakati na mafundisho ya Imam Husayn (a.s.).
Alisema Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei aliishi maisha yaliyofungamana kikamilifu na njia ya Imam Hussein (a.s.), akifikiri, akiongoza, akipambana na kujitolea kwa roho ya Husayni hadi alipofikia daraja la juu la shahada katika kulitumikia dini ya Mwenyezi Mungu.
Kiongozi huyo alieleza kuwa damu ya mashahidi huamsha Umma wa Kiislamu na kuunganisha kila zama na tukio la Ashura pamoja na ardhi ya Karbala. Aliongeza kuwa maombolezo na mazishi ya Imam Shahidi yamekuwa ni mwendelezo wa mwito wa Imam Husayn (a.s.) wa "Je, yupo wa kuninusuru?", ambao umeamsha mamilioni ya watu nchini Iran, Iraq na katika maeneo mengine ya ulimwengu.

Katika tamko hilo, Ayatullah Sayyid Mujtaba al-Husseini Khamenei aliwashukuru mamilioni ya wananchi waliojitokeza katika mazishi yaliyofanyika katika miji mbalimbali ya Iran na Iraq, hususan Tehran, Qom, Mashhad, Najaf na Karbala, akieleza kuwa ushiriki huo mkubwa umeonesha mshikamano wa Umma wa Kiislamu na umewavunja moyo maadui.
Aidha, aliahidi kuwa njia na shule ya Imam Shahidi italindwa na kuendelezwa kwa uthabiti, huku akisisitiza kuwa damu yake pamoja na damu za mashahidi wengine haitapotea bure. Alisema kuwa wahusika wa mauaji hayo watawajibishwa, na kwamba kutafuta haki kwa damu za mashahidi ni matakwa ya wananchi wa Iran ambayo, kwa mujibu wa tamko hilo, yatatimia.
Mwishoni mwa ujumbe wake, Ayatullah Sayyid Mujtaba al-Husseini Khamenei alimwomba Mwenyezi Mungu awape mashahidi daraja za juu, awajaalie subira familia zao, na ailinde Iran pamoja na kuijaalia ushindi wa karibu, huku akitoa salamu na rambirambi kwa Imam wa Zama, Imam al-Mahdi (a.f.).

Your Comment