Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-; Karne kumi na nne zilizopita, katika usiku wa 19 wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ambaye ni mkwe, binamu na mtu wa karibu sana kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), alipigwa upanga uliokuwa umepakzwa sumu kali kupindukia na kujeruhiwa vibaya kichwani mwake akiwa katika ibada ya Swala ya Alfajiri katika Msikiti wa al-Kufa huko Iraq.
Imam Ali (a.s) alipigwa upanga na mtu aliyejulikana kwa jina la Abdur Rahman bin Muljim Muradi (laana iwe juu yake milele). Imam Ali (a.s) alikufa Shahidi siku tatu baadaye katika usiku wa 21 wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ni shakhsia wa pili mkubwa katika Uislamu baada ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), na anaelezwa katika historia ya Uislamu kuwa alikuwa jasiri na shujaa wa kupigiwa mfano, mwenye imani thabiti, mwenye akhlaki njema, mwenye elimu na uadilifu usio na kifani.
Elimu ya Imam Ali (a.s) na Ushujaa Wake
Imam Ali bin Abi Talib (a.s), alipata elimu na kulelewa katika nyumba ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w). Hivyo yeye ni Mwanafunzi wa Kwanza wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na alikuwa Mwanamume wa kwanza kuukubali Uislamu na kumfuata Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Lakini pia Imam Ali (a.s) yeye ni Shujaa wa Uislamu. Na ndiye mwenye Lakabu ya SIMBA WA MWENYEZI MUNGU MWENYE KUSHINDA. Hakuna adui ayekuwa na ubavu mbele ya upanga na nguvu za Imam Ali (a.s). Alikuwa mkali vitani kama Simba. Historia ya vita vya Khaybar ni kielelezo tosha cha uwezo na nguvu zake vitani, na ndiye aliyweza kuiporomosha ngome ya mayahudi wa khaybari na akarudi kwa Mtume (s.a.w.w) akiwa na ushindi mkubwa.
Kumbuka kabla yake Mtume (s.a.w.w) alituma masahaba kadhaa (na historia imetaja majina yao), lakini walishinda kuifungua ngome ya mayahudi wa khaybari, lakini Imam Ali (a.s) alipopewa na Mtume (s.a.w.w) Bendera ya Kiislamu na kumtuma kwenda kuikomboa ngome hiyo, mayahudi walipata chamtema kuni, na walikumbana na nguvu za kivita za Imam Ali (a.s), aliyeiporomosha ngome hiyo na mayahudi wakajisalimisha mbele yake na kuinua mikono kama ishara ya kushindwa vita hiyo mbele ya mapambano ya Simba wa Mwenyezi Mungu, Ali bin Abi Talib (a.s).
Katika vipindi tofauti daima Imam Ali (a.s) alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume (s.a.w.w) katika hali zote za shida na matatizo, na alihatarisha maisha yake (alijitoa muhanga nafsi yake) ili kumlinda Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na dini ya Uislamu alipofanya tukio la kulala katika Kitanda cha Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), ili maadui waliokuwa wakimvizia kumuua Mtume (s.a.w.w) wakija wasimkute Kitandani na bora wamuue yeye lakini ahakikishe uhai na maisha ya Mtume (s.a.w.w) yanakuwa salama kwa ajili ya Dini Tukufu ya Kiislamu. Kutokana na tukio hilo, Allah (s.w.t) akaremsha Aya tukufu katika haki ya Imam Ali (a.s) ambapo alisema:
«وَمِنَ النَّاسِ مَن یَشْرِی نَفْسَهُ ابْتِغَاء مَرْضَاتِ اللّهِ وَاللّهُ رَؤُوفٌ بِالْعِبَاد» (بقرة/207)
"Na katika watu yupo auzaye nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja" (Surat Al-Baqarah: Aya ya 207).
Aya hii Tukufu imeshuka ikimhusu Ali bin Abi Talib (a.s). Na suala hili la kujitoa (au kuitanguliza) nafsi yako kwa ajili ya wengine (ithar) ni katika sifa bora na juu zaidi za Mwanadamu. Sifa hii alipambika nayo Imam Ali (a.s) kwa ukamilifu zaidi alipoitoa muhanga nafsi yake kwa ajili ya kuhifadhi uhai na maisha ya Bwana Mtume (s.a.w.w), na kwa ajili Dini Tukufu ya Kiislamu.
Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali (a.s) alikuwa mpole na mwenye upendo na huruma. Imam Ali (a.s) daima alitetea Haki na Uadilifu na kupambana ipasavyo na dhulma katika kila njanya.
Usiku Ulioahidiwa
Katika usiku ule ulioahidiwa, Amiri wa mema na matukufu, Ali bin Abi Talib (a.s) alikuwa akitoka nje ya nyumba mara kwa mara na kuangalia juu mbinguni. Alionekana akifanya istighfari na kusoma Surat Yasin. Usiku ule Sala, Dua na Maombi ya Imam Ali (a.s) yalitofautiana na ya nyusiku zingine na daima alikuwa akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Nibarikie mimi mauti."
Baadhi ya Waumini walikuwa wamenza kuelekea Msikitini kwa ajili ya Sala ya Alfajiri. Imam Ali (a.s) kama kawaida yake, alitoka haraka na kuelekea Msikitini. Baada ya kuingia Msikitini katika Mji waal-Kufa, Iraq katika hali ya giza. Baada ya kufika Msikitini alisali rakaa kadhaa na kisha akapanda juu ya mnara wa Msikiti na kuanza kutoa adhana. Allahu Akbar... Allahu Akbar...
Muda mfupi baadaye Imam Ali (a.s) alisimama kwa ajili ya sala ambayo ilitawaliwa na hali isiyokuwa ya kawaida. Hakika siku iliyoahidiwa ilikuwa imewadia. Ibn Mujlim, Mwanadamu muovu zaidi kuliko wote, alikuwa amezama katika fikra za giza na upotovu. Alijongea kwa Imam Ali (a.s) aliyekuwa katika Sala na kumpiga kichwani kwa upanga uliokuwa na sumu kali. Upanga huo wenye sumu kali ulizama katika kichwa cha Imam Ali (a.s) hadi sehemu ya mbele ya kusujudia. Hakika upanga huo ulitayarisha mazingira ya kutenganisha Umma na Kiongozi wake Kipenzi na kuwatia simanzi na majonzi yasiyokuwa na kifani Waumini waliokuwa wakimzunguka kama nyuki watafutao asali.
Ninaapa Kwa Jina la Mola wa al-Kaaba
Katika kipindi hicho ambapo Imam alikuwa amelala katika damu juu msala wa mahaba na kumpenda Mwenyezi Mungu, alionja ladha ya uhuru wa kuondoka katika dunia hii finyu na ya kupita na kuwasiliana na Mola Mlezi wake. Hakika alikuwa amevuka kipindi cha maumivu ya kimwili na kuona ahadi aliyokuwa amepewa na Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) ikitimia. Aliinua kichwa mbinguni na kusema: "Ninaapa kwa jila la Mola wa al Kaaba kwamba hakika nimefuzu."
Imepita miaka bali karne nyingi sasa ambapo wasomi, wanazuoni na wahakiki wamekuwa wakizungumza na kuandika mengi kuhusu shakhsia ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s). Vitabu vingi vya nathari na mashairi vimeandikwa katika kutaja wasifu wa mtukufu huyo ambaye ndiye wa kwanza kuzaliwa ndani ya nyumba tukufu ya al Kaaba. Ali bin Abi Talib (a.s) alikuwa Mwanaume wa kwanza kukubali wito wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) na wa kwanza kumfuata Mtume katika sala ya jamaa. Tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi alikuwa akienda pamoja na Mtume SAW katika jangwa la kandokando ya Makka na kunong'ona na Mola Muumba, na mwenendo huo wa kumtaradhia na kumuomba Mwenyezi Mungu kwa siri aliuendeleza hadi alipopigwa upanga kichwani akiwa katika sala msikitini.
Imam Ali (a.s) alikuwa akifanya ibada zaidi ya watu wote
Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) alifupisha sifa na matukufu ya Ali bin Abi Talib (a.s) katika sentensi fupi pale aliposema: "Ali amevutwa na kuzama katika upendo wa dhati ya Mwenyezi Mungu." Katika sehemu nyingine Mtume (s.a.w.w) anasema: "Lau kama mbingu na ardhi zote vitawekwa katika upande mmoja wa mizani na imani ya Ali bin Abi Twalib ikawekwa katika upande wa pili, basi upande wa imani ya Ali utakuwa mzito zaidi."
Mwanahistoria na A'limu Mashuhuri wa Madhehebu ya Sunni Ibn Abil Hadid ameandika yafuatayo kuhusu ibada na dua za Ali bin Abi Talib (a.s), anasema:
"Alikuwa akifanya ibada zaidi ya watu wote na kusali swala za usiku na kufunga saumu nyingi kuliko wengine. Aliwafunza watu kusali sala za usiku na jinsi ya kusali sala za sunna.... paji lake la uso liliota nundu kutokana na kusujudu sana."
Ibnu Abil Hadid anaendelea kusema kuwa: "Unapotafakari katika dua na minong'ono yake na Mola Muumba na kuzama katika maana za kina zilizomo katika dua hizo kuhusu jinsi anavyomuadhimisha Mwenyezi Mungu na kunyeyekea mbele ya haiba yake, ndipo utakapoelewa kiwango cha ikhlasi ya mtukufu huyo(Ali bin Abi Talib -a.s-). Hapa utapata kuelewa dua na maombi hayo yalikuwa yakitoka katika roho kubwa kiasi gani ..."
Maarifa na Elimu Kubwa ya Ali bin Abi Talib (a.s)
Maarifa na elimu kubwa ya Ali bin Abi Talib (a.s) kuhusu Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndio chanzo cha upendo na hisi yake ya kupigania uadilifu na haki.
Imam Ali (a.s) aliitambua vyema nafsi yake na huu ulikuwa msingi wa maarifa ya juu, yaani maarifa ya kumjua Mola Muumba na Mkamilifu Mutlaki. Imam Ali (a.s) alikuwa akisema: "Dunia na vilivyomo haiwezi kufikia nafasi aali (ya juu) ya Mwanadamu, na hadhi ya Mwanadamu iko juu kiasi kwamba haiwezi kuuzwa kwa thamani ya dunia, kwani dunia ni wenzo na chombo cha kutumia kwa ajili ya kufikia makazi halisi ya Mwanadamu." Alikuwa akisema: "Sikuona kitu chochote ila nilimuona Mwenyezi Mungu kabla yake, baada yake na pamoja nacho."
Ni maarifa haya ya kina ndiyo siri ya dua na minong'ono ya Imam Ali (a.s) na Mola wake Mlezi. Pamoja na hayo dua na ibada hizo za Imam hazikumzuia kufanya kazi na bidii ya kustawisha nchi, kupigana jihadi katika njia ya Allah, kupambana na dhulma na kupigania haki na uadilifu. Si hayo tu, bali Imam aliyatambua hayo kuwa ni ibada kubwa zaidi. Alimkumbuka Mwenyezi Mungu katika hali zote na hakughafilika na Mola wake hata lahadha moja. Katika moja ya hotuba zake ndani ya Nahjul Balagha, Imam Ali anataja sifa za wacha-Mungu ambaye yeye mwenyewe ni kinara wao akisema: Wameonja tamu ya maarifa ya Mwenyezi Mungu na kukata kiu yao kwa bilauri ya upendo na mahaba ya Mola wao, matokeo yake wamejielekeza katika twaa na uja kiasi kwamba migongo yao imepinda kutokana na wingi wa ibada.
Kughiriki na Kuzama Katika Ibada
Imepokelewa kwamba Imam Ali (a.s) alijeruhiwa vitani kiasi kwamba mshale ulizama ndani ya mfupa wake na kusababisha maumivu makali. Matabibu walijitahidi kadiri ya uwezo kuondoa mshale huo katika mguu wa Imam lakini hawakuweza. Tabibu mmoja alisema mshale huu hauwezi kutoka bila ya kupasua nyama na eneo hili. Jamaa wa Imam na watu wa karibu yake walisema, kama hapana budi ya kupasua sehemu mshale huo ulipoingia, basi subirini hadi atakapoingia katika ibada ya sala na kunong'ona na Mola wake, wakati huo mtaweza kutoa mshale huo. Walisisitiza kwamba Imam Ali (a.s) anapokuwa katika ibada ya sala hughiriki katika ibada na kuondoka kabisa katika dunia hii. Matabibu walisubiri hadi Imam alipoanza kuswali na kughiriki katika ibada, wakati huu ndipo walipoweza kuondoa mshale ule bila hata ya Imam mwenyewe kuhisi.
Tunahitimisha Makala yetu kwa moja ya kauli zenye hekima za Imam Ali bin Abi Talib (a.s) aliposema:
«والله لأن أبيت على حسك السعدان مسهّداً وأُجرّ في الاغلال مصفّداً أحبّ إليَّ من أن ألقي الله ورسوله يوم القيامة ظالماً لبعض العباد...»
"Naapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu kwamba, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w) Siku ya Kiyama hali ya kuwa nimewadhulumu baadhi ya waja wake."
Ogopa kumdhulumu mja wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) haki yake anayoistahiki.
Tunatoa salam za pole kwa Waislamu wote Ulimwenguni hususan Wapenzi na Wafuasi wa Ahlul Bayt (a.s) ambao ndio Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) kutokana na mnasaba huu mchungu wa kukumbuka tukio chungu la Kuuawa Kishahidi Imam wa Wacha Mungu, Amirul Muuminina, Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yake).
Your Comment